Udhibiti waimarishwa utoaji stika za usalama barabarani

Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Pwani, Edward Gontako akizungumza wakati wa ukaguzi wa magari leo Jumapili Oktoba 22,2017. Picha na Julieth Ngarabali.

Muktasari:

  • Stika kuwa na namba maalumu kwa kila eneo.

Katika kudhibiti ukaguzi wa magari na mapato, utoaji wa stika za usalama barabarani utafanyika kwa kila eneo kuwa na namba zake, imeelezwa.

Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Pwani, Edward Gontako amesema utaratibu huo utawezesha kubaini gari limekaguliwa katika wilaya gani na kujua mapato halisi kwa kila eneo.

Gontako amewataka madereva na wamiliki wa magari watakaotia shaka stika watakazopewa na askari wa usalama barabara kutoa taarifa.

Amesema uchunguzi utafanyika na ikibainika kuwa ni stika bandia hatua za kisheria zitachukuliwa kwenye eneo husika.

Amesema hayo leo Jumapili Oktoba 22,2017 wakati wa uzinduzi wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani mkoani Pwani.

Magari zaidi ya 100 yakiwemo ya wanafunzi, mabasi na ya binafsi yamekaguliwa, na mengi yamebainika kutokuwa na mikanda na ni mabovu.

"Stika zitatolewa kwa Sh5,000 ila tofauti na miaka mingine, mwaka huu hazitolewi holela, kila wilaya ina namba yake kwa hiyo tukikamata gari tunajua limekaguliwa wapi  na kama lina shida tunajua tumkamate askari yupi. Pia hata mapato tutajua eneo fulani wameuza kiasi gani," amesema Gontako.

Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jonathan Shanna alisema matukio ya ajali mkoani humo yamepungua kutoka 112 kwa kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka jana hadi 31 kipindi kama hicho mwaka huu, sawa na asilimia 72.2 .

Kamanda Shanna amesema dhamira ya wiki ya nenda kwa usalama ni kuhakikisha magari yote yanayotembea barabarani ni mazima kwa kuwa ni hatari kutumia chombo cha moto kibovu.

Amesema wataendelea kutoa elimu kwa watumiaji na wamiliki wa magari ili kujenga tabia ya kutoa taarifa wakibaini gari ni bovu, dereva anakwenda mwendo usiojali maisha ya abiria na lugha chafu.