Marais wanane kushuhudia Weah akiapishwa

Muktasari:

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Protokali, Jarvis Witherspoon imesema maofisa wengine waliothibitisha kuhudhuria ni ujumbe maalum kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) na kutoka Marekani, Ufaransa na Umoja wa Mataifa (UN).

 

 

 

Monrovia, Liberia. Wakuu wanane wa nchi za Afrika wamethibitisha kuhudhuria sherehe za kuapishwa George Weah kuwa na rais na makamu wake Jewel Howard-Taylor kesho jijini hapa akiwa rais wa 24 wa Liberia.

Wakuu wa nchi waliothibitisha ni Jacob Zuma wa Afrika Kusini; Faure Gnassingbe wa Togo; Muhammadu Buhari wa Nigeria; Alpha Conde wa Guinea; Nana Akufo-Addo wa Ghana; Ernest Bai Koroma wa Sierra Leone; Jose Mario Vaz wa Guinea Bissau; na Ali Bongo Ondimba wa Gabon.

Weah na makamu wake Howard-Taylor wanatarajiwa kuapishwa kesho katika sherehe za kufana wakipokea kijiti cha uongozi kutoka kwa manamama Ellen Johnson Sirleaf. Sherehe hizo zitafanyika kwenye Uwanja wa Michezo wa Samuel K. Doe (SKD).

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Protokali, Jarvis Witherspoon imesema maofisa wengine waliothibitisha kuhudhuria ni ujumbe maalum kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) na kutoka Marekani, Ufaransa na Umoja wa Mataifa (UN).

Witherspoon aliweka wazi ugeni huo alipozungumza na wanahabari kwenye ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje ambapo alisema wabunge wa Bunge la 53 na 54, wanasoka, na maofisa wa serikali watahudhuria.

Kwa minajili ya usalama, chama tawala cha CDC kitagawa tiketi za kuingilia zipatazo 15,000, maofisa wa serikali watapewa tiketi 5,000. Vyama vya kiraia, wanadiplomasia, maofisa wa zamani wa serikali na raia wengine wa Liberia watapewa tiketi waweze kushuhudia tukio hilo linalotajwa kuwa la aina yake.