Marais wapya barani Afrika washiriki UNGA

Muktasari:

  • Wakuu wengine walioanza kuwasili jijini kwa ajili ya mkutano huo ni Peter Mutharika wa Malawi na Yoweri Museveni wa Uganda, Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Muhammadu Buhari wa Nigeria, Paul Biya wa Cameroun, Denis Sassou Nguesso wa Congo.

Marais watatu wapya Afrika wanatarajiwa kuwa miongoni mwa wakuu wa nchi kadhaa kutoka bara hilo watakaohudhuria kwa mara ya kwanza wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) tangu walipochaguliwa mwaka huu.

Wakuu wengine walioanza kuwasili jijini kwa ajili ya mkutano huo ni Peter Mutharika wa Malawi na Yoweri Museveni wa Uganda, Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Muhammadu Buhari wa Nigeria, Paul Biya wa Cameroun, Denis Sassou Nguesso wa Congo.

Marais hao ni kutoka Ghana, Gambia na Somalia. Tofauti na wenzake, Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo hatakuwa mgeni sana na mikutano ya UNGA kwani alikuwa kuwa waziri wa mambo ya nje, lakini kama rais itakuwa mara ya kwanza kuhudhuria mkutano huo wa 72.

Nana alishinda urais baada ya kumwangusha rais aliyekuwa anatetea nafasi yake John Mahama katika uchaguzi uliofanyika Desemba 7. Ilikuwa mara yake ya tatu kuwania urais baada ya kushindwa mwaka 2008 na mwaka 2012.

Rais wa Gambia, Adama Barrow utakuwa uzoefu wake wa kwanza kuhudhuria mkutano huo baada ya kumshinda rais wa muda mrefu Yahya Jammeh Desemba 1, 2016. Barrow, ambaye alitokana na muungano wa upinzani alimshinda Jammeh kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotolewa na tume ya uchaguzi.

Jammeh alikubali kushindwa kabla ya kubadilika na kudai hakushindwa akitaja dosari kadhaa wakati wa ujumlishaji matokeo na akakataa kukabidhi madaraka. Hata hivyo, baada ya Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (Ecowas) kushindwa kumshawishi Jammeh kuondoka mamlakani, iliamua kutumia nguvu na akaridhia kabla majeshi hayajaingia.

Kuhusu Rais wa Somalia, Mohamed Abdullahi Farmaajo, ripoti zinaonyesha atamtuma Waziri Mkuu, Hassan Ali Khaire kumwakilisha. Khaire ndiye alimwakilisha Rais katika mkutano wa Umoja wa Afrika, Addis Ababa uliofanyika Januari.