Marasta kupewa vitambulisho Ethiopia

Muktasari:

  • Marasta hao wamefurahia uamuzi wa Serikali ya Ethiopia na kusema kwamba ndoto yao ya kuifanya Afrika moja inaweza kutimia.

Marasta wapatao 1,000, ambao wamekuwa hawana uraia wa nchi yoyote, watapewa vitambulisho na Ethiopia, kwa mujibu wa taarifa ya Serikali ya nchi hiyo iliyotolewa jana.

Marasta wapatao 1,000 wanaishi Ethiopia, hasa mji mkuu wa Addis Ababa na mji wa Shashamane ulio Kaskazini baada ya mfalme wa zamani, Haile Selassie kutoa ardhi eneo la Shashamane kwa ajili ya kuishi watu weusi.

Imani ya kirasta, ambayo ilianza baada ya mfalme huyo kuingia madarakani, ina waumini ambao wanaamini kuwa mfalme huyo ni mungu.

Marasta hao sasa wanaweza kuingia Ethiopia bila ya viza na kuishi bila ya kuhitaji vibali vya uhamiaji baada ya Serikali kufanya uamuzi huo ambao pia unahusu wayahudi wenye asili ya Ethiopia na raia wengine wa kigeni ambao wamekuwa na mchango mzuri kwa taifa hilo, tovuti ya abcnews imeandika leo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Meles Alem alisema: “Kwa suala la Marasta, tuna vizazi vitatu vya watu ambao wanaishi hapa na wameelewana na wenyeji. Lakini kwa bahati mbaya hawakuwa Wacarribean wala Waethiopia, kwa namna fulani walikuwa hawana uraia wowote. Vitambulisho hivi vitatatua tatizo hilo," alisema Alem.

Taarifa hizo zimefurahisha Marasta.

“Tuna furaha kupita kiasi,” alisema Ras King, mmoja wa watu maarufu katika Jumuiya ya Marasta ambaye aliingia Ethiopia kwa mara ya kwanza mwaka 1982.

“Tuna furaha sana kwa sababu hili limeongeza imani yetu kwa ndoto ya mababa zetu ya kuwa na Afrika moja na watu weusi kutoka Magharibi. Kama kawaida, Ethiopia imeongoza njia na kuweka mfano kwa wengine barani kutambua harakati za marasta.”