Marekani yaipa TZ Sh850 bilioni

Muktasari:

Hatua hiyo imekuja wakati hivi karibuni Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) ilitangaza kuinyima Tanzania msaada wa Dola 473 milioni (zaidi ya Sh1 trilioni), kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kuvunjwa kwa misingi ya kidemokrasia.

Dar es Salaam. Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa (UsAid), imetoa msaada wa Sh854.7 billioni kwa ajili ya kusaidia sekta za afya, kilimo, usimamizi wa maliasili, nishati na utawala wa bora.

Hatua hiyo imekuja wakati hivi karibuni Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) ilitangaza kuinyima Tanzania msaada wa Dola 473 milioni (zaidi ya Sh1 trilioni), kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kuvunjwa kwa misingi ya kidemokrasia.

Mkurugenzi Mkazi wa UsAid nchini, Sharon Cromer na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk Servacius Likwelile jana walisaini mkataba wa miaka mitano wa makubaliano ya mageuzi ya uchumi na huduma za jamii.

“Marekani inalenga kuisaidia Tanzania kufikia azma yake ya mageuzi ya uchumi na jamii, kuwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025,” alisema Cromer.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubya alisema fedha hizo zitasaidia kuboresha huduma za jamii nchini.