Marekani yapinga Saudi Arabia kumwalika Rais Bashir

Marekani imesema haiungi mkono hatua ya Serikali ya Saudi Arabia kumwalika Rais Omar al-Bashir wa Sudan kushiriki katika mkutano wa nchi za kiarabu kesho Jumapili ambao utahudhuriwa pia na Rais Donald Trump.

Ubalozi wa Marekani jijini umesisitiza kuwa hauungi mkono mwaliko aliopewa mtu ambaye anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Hii itakuwa ni ziara ya kwanza kwa Rais Trump nje ya nchi yake tangu alipoingia madarakani Januari mwaka huu lakini tayari imeanza kujadiliwa vikali kutokana na mwaliko aliopewa pia Bashir lakini pia hatua yake ya kuzuia raia kutoka mataifa saba ya Kiislamu kwenda Marekani, agizo ambalo hata hivyo lilizuiwa na mahakama.

Bashir anatafutwa na ICC kwa kuchochea na kufadhili mauaji ya zaidi ya watu 300,000 katika jimbo la Darfur. Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Ibrahim Ghandour amethibitisha kuwa Rais Bashir atakwenda katika mkutano huo.

Akiwa Saudi Arabia, Trump atawahutubia ulimwengu wa Kiarabu kuhusu umuhimu wa amani katika nchi za Kiislamu.