Masauni: Msimamo ni kutoagiza viatu nje

 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni.

Muktasari:

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alipotembelea kiwanda hicho kilichopo mjini Moshi mkoani humo.

Moshi. Serikali imesisitizia msimamo wake wa kutoruhusu uagizwaji wa viatu kutoka nje ya nchi kwa ajili ya majeshi na badala yake vitazalishwa na kusambazwa na kiwanda pekee cha viatu cha Jeshi la Magereza cha mkoani Kilimanjaro.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alipotembelea kiwanda hicho kilichopo mjini Moshi mkoani humo.

“Ili kumuunga mkono Rais John Magufuli aweze kufikia lengo la kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati na ya viwanda, nitahakikisha nalifuatilia hili agizo na utekelezaji alilolitoa kwa kumuunga mkono kwa kufufua viwanda vyetu vya ndani,” alisema Naibu Waziri huyo.

Alisema lengo la ziara yake kiwandani hapo ni kuona hatua waliyofikia baada ya maelekezo yaliyotolewa na Rais Magufuli ya kutaka kuendelea kutumia kiwanda hicho cha Magereza kuzalisha bidhaa za ngozi na hususan viatu.

Kaimu Mkuu wa kiwanda hicho, Michael Minja alisema kina uwezo wa kuzalisha viatu 250 kwa siku na kwa sasa wanaoda ya viatu jozi 15,000 vya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) .