Mashahidi waitwa Ikulu, kesi yakwama kusikilizwa

Muktasari:

Leo Ikulu jijini Dar es Salaam Rais John Magufuli alikutana na viongozi wa TFF na baadhi ya wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania

 

Dar es Salaam. Kesi  ya kula njama na kughushi  inayomkabili aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),  Jamal Malinzi na wenzake wa wanne imekwama kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  baada ya mashahidi kuitwa Ikulu na Rais John Magufuli.

Hayo yameelezwa leo na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri wakati wa kesi hilo ilipotajwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi upande wa Jamhuri.

Oktoba 16 kesi hiyo iliahirishwa baada ya wakili Kimaro kuiomba mahakama impe muda apitie mwenendo wa kesi kwa sababu ilikuwa inaendeshwa na wakili mwingine wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Leo Ikulu jijini Dar es Salaam Rais Magufuli alikutana na viongozi wa TFF na baadhi ya wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania.

Kimaro amedai mashahidi ambao alikuwa anawategemea kufika kwa ajili ya kutoa ushahidi wameitwa Ikulu.

"Kesi ilikuja kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji na mashahidi ambao tulisha waandaa wameitwa  na Rais Magufuli Ikulu hivyo tunaomba tarehe nyingine ili tuweze kuendelea," ameeleza  Kimaro.

Upande wa mashtaka baada ya kuwasilisha hoja hizo, wakili wa utetezi, Richard Rweyongeza alilalamika kwamba hoja ambazo zimetolewa na wakili Kimaro zinaonyesha ni dharau kwa sababu kesi hiyo ina mashahidi wengi ambao sio wote waliitwa Ikulu.

"Naomba upande wa mashitaka wajitahidi kutuletea mashahidi wa kutosha ili kesi iweze kuendelea kuliko kusubiri mashahidi hao tu,” alisema.

Hakimu Mashauri baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, aliuagiza  upande wa mashitaka  kupeleka mashahidi wa kutosha Oktoba 30 na Novemba Mosi kesi hiyo itakapoendelea na usikilizwaji ushahidi .

Mbali na  Malinzi,  washtakiwa wengine  ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine na Mhasibu wa TFF,  Nsiande Mwanga.

Wengine ni meneja wa  ofisi ya TFF, Miriam Zayumba na karani wa shirikisho hilo, Flora Rauya ambao kwa pamoja  wanakabiliwa na mashtaka 30 katika  kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha dola za Marekani 173,335 na Sh43,100,000.

Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wapo rumande kwa mashtaka ya utakatishaji wa fedha ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana, huku wenzao Zayumba na Frola wakiwa nje kwa dhamana.

 

Tayari mashahidi nane wa upande wa mashtaka wamekwishatoa ushahidi  wao.