Mashahidi wakwamisha kesi ya bilionea Msuya

Muktasari:

Hata hivyo, jana kesi kuu ilitakiwa kuendelea lakini ikakwama kwa sababu mashahidi waliotarajiwa walishindwa kufika mahakamani.

Jaji Salma Maghimbi amekubali kupokea ungamo la mshtakiwa wa tano, Karim Kihundwa baada ya mwenyewe kudai kuwa alilazimishwa kusaini maelezo hayo akituhumiwa kuhusika kwenye mauaji ya mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite, bilionea Erasto Msuya.

Hata hivyo, jana kesi kuu ilitakiwa kuendelea lakini ikakwama kwa sababu mashahidi waliotarajiwa walishindwa kufika mahakamani.

Kushindwa kufika kwa mashahidi hao wawili, kulisababisha Jaji Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi kuiahirisha hadi Jumatatu.

Wakili wa Serikali, Abdallah Chavula alilazimika kuiomba mahakama iahirishe kesi hiyo baada ya mashahidi hao kupata dharura wakiwa njiani.

Pia, ombi hilo lilikubaliwa na mawakili wa utetezi wanaoongozwa na Majura Magafu, John Lundu, Emmannuel Safari na Hudson Ndusyepo huku wakitoa angalizo kuwa wakati mwingine upande wa mashtaka uhakikishe unaleta mashahidi wa kutosha.

Akiahirisha kesi hiyo, Jaji Maghimbi aliutaka upande wa mashtaka kuhakikisha Jumatatu unaleta mashahidi wengi zaidi ili kuepuka usumbufu wa kuahirisha kesi bila sababu za msingi.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Sharifu Mohamed, Shaibu Said (Mredii), Mussa Mangu, Jalila Zuberi, Kihundwa, Sadik Mohamed na Ally Mussa ambao inadaiwa Agosti 7, 2013 walimuua Msuya eneo la Mijohoroni wilayani Hai.

Akitoa uamuzi wa kesi ndani ya kesi, Jaji Maghimbi alimaliza mvutano ulioibuka kwenye kesi kuu na kukubali kupokea maelezo ya maungamo ya mshtakiwa Kihundwa kama kielelezo.

Baada ya Jaji Maghimbi kupokea kielelezo hicho, shahidi wa 12 Ponsian Claud alilisoma ungamo hilo mahakamani neno kwa neno.

Wakili wa Serikali, Omary Kibwana alimwambia shahidi huyo asome maelezo ya mshtakiwa.

Shahidi alianza kusoma maelezo hayo ifuatavyo:- Mimi Karim Issah Kihundwa nilipigiwa simu na Sadik kuwa kuna mtu ananisubiri kutoka Arusha, Bwana Sharifu na kwamba kuna kazi anataka kunipa.

Nilipofika Arusha, Sadik aliniambia kuna kazi wanataka kunipa ya kumuua bilionea Erasto Msuya. Baada ya hapo Sharifu alinipa silaha kisha tukaelekea msituni kwenda kufanya majaribio ya kufyatua risasi.

Baada ya hapo, Sharifu alirudi katika chumba cha wageni alichokuwa amechukia.

Kesho yake asubuhi, Sharifu na Mredii walirudi tena Arusha ndipo tukajipanga kurudi Moshi na tulipofika maeneo ya Mijohoroni, Sharifu aliniambia kuna tajiri mmoja anakuja anaitwa bilionea Erasto Msuya huyo ndiyo nataka umuue.

Sharifu aliniambia atakuja na mwenzake, lakini Erasto Msuya amevaa cheni za gold (dhahabu)nyingi shingoni mwake na amevaa miwani myeusi.

Erasto Msuya alivyofika pale Mijohoroni katika lile eneo ambalo tulikubaliana tukutane naye, alivyoshuka tu kwenye gari nilimfyatulia risasi kisha kumuua, baada ya hapo zilikuja pikipiki mbili tukakimbilia msituni sehemu ambayo tulikuwa tumepanga tukutane baada ya kumaliza kumuua Erasto, na baada ya hapo Sharif alinipa Sh1 milioni.

Siku iliyofuata Sadiki aliniambia kuwa Sharifu amekamatwa na sisi tunatafutwa. Baada ya kunipa ile Sh1 milioni aliniambia leo ni siku ya Iddi siwezi kufanya lolote.

Mimi siku ya Jumatano nilikwenda shambani kwangu Ngage kwenda kuangalia shughuli zangu za kilimo baada ya muda nilikuja kukamatwa.

Baada ya kusoma maelezo hayo, wakili Magafu alianza kumhoji shahidi huyo kama ifuatavyo:-

Wakili Magafu: Baada ya kukabidhi maelezo yale yakiwa kwenye bahasha nini ulifanya?

Shahidi: Niliendelea na majukumu yangu kama kawaida.

Wakili Ndusyepo: Ulishawahi kupata malalamiko ya watu waliowekwa chini ya ulinzi wanapigwa?

Shahidi: Hakuna aliyewahi kuniletea malalamiko.

Wakili Ndusyepo: Mahakama ya mwanzo unashughulika na kesi za mauaji?

Shahidi: Ndiyo.

Wakili Ndusyepo: Uliwahi kupata mashtaka madogo madogo kama wizi wa kuku ukayashughulikia?

Shahidi: Ndiyo.

Wakili Ndusyepo: Wanakuwa na hali gani?

Shahidi: Kawaida.

Wakili Ndusyepo: Hakuna washtakiwa waliowahi kufikishwa kwako kwenye kesi ya mauaji wakiwa wamepigwa?

Shahidi: Wapo.

Wakili Ndusyepo: Ebu isaidie mahakama hii, mshtakiwa aliyeletwa kwako na polisi Septemba 17, 2013 ni kitu gani zaidi uli test (jaribu) kujua huyu mtu yuko kwenye maumivu ya mwili.

Shahidi: Nilimwangalia tu hali yake aliyokuwa nayo.

Wakili Ndusyepo: Uliwahi kukutana na mtu mwingine ambaye yuko chini ya ulinzi wa polisi kwa muda mrefu?

Shahidi: Sijawahi kukutana naye.

Wakili Ndusyepo: Uliieleza mahakama hii kwamba Inspekta Samwel alikuja na mshtakiwa ofisini kwako, akina afande Atway walikuwa wamejificha wapi?

Shahidi: Ndiyo kwanza namsikia huyo Inspekta Atway.

Wakili Ndusyepo: Sehemu ambazo zilikuwa na utata katika ile karatasi ya maungamo wewe ulifanya nini, ukiwa unamsomea yale maelezo ulipata kumuuliza swali?

Shahidi: Niliandika maelezo yake, sina nafasi ya kumhoji wakati namsomea maelezo.

Wakili Ndusyepo: Ebu tutengulie kitendawili hiki hapa, kuna nyaraka ulisema wewe uliandika, kitu gani kinaonyesha ukurasa wa pili inaunganika na ukurasa wa kwanza na wa tatu?

Shahidi: Mtiririko wa maswali na majibu.

Wakili Ndusyepo: Je, zilikua na tarehe?

Shahidi: Karatasi ya kwanza ilikuwa na tarehe.

Wakili Ndusyepo: Karatasi ya pili?

Shahidi: Ilikiwa haina tarehe.

Wakili Ndusyepo: Karatasi ya tatu je?

Shahidi: Ilikuwa ina tarehe.

Wakili Ndusyepo: Ni kitu gani kinaonyesha kuwa karatasi ya tatu na ya kwanza ziko sawa.

Shahidi: Karatasi ya pili ina item namba mbili ambayo inaenda na ya kwanza hadi ya tano.

Wakili Ndusyepo: Mwendelezo wako wa karatasi una kurasa na umeandika katika kueleza hicho, Ebu onyesha ni wapi karatasi zina ukurasa?

Shahidi: Hazikuwa na page (kurasa) namba.

Wakili Ndusyepo: Inspekta Samwel ilikuwa mara yako ya ngapi kumuona?

Shahidi: Ilikuwa ni mara ya kwanza.

Wakili Ndusyepo: Alijitambulisha kama nani kwako?

Shahidi: Alijitambulisha kama Inspekta wa Jeshi la Polisi.

Wakili Ndusyepo: Uliona kitambulisho chake au alivaa sare za jeshi?

Shahidi: Hakuwa na kitambulisho wala sare za jeshi.

Wakili Ndusyepo: Kwa hiyo ulimwamini kweli, siyo kweli?

Shahidi: Siyo kweli.

Wakili Ndusyepo: Ni kweli kwamba Inspekta Samwel alikuwa anafika mahakamani hapo mara kwa mara na gari ya DFP?

Shahidi: Siyo kweli.

Wakili Ndusyepo: Nani alikwambia kuwa mshtakiwa anataka kuandika maelezo ya ungamo mbele yako?

Shahidi: Hakimu Anitha Mkau na Inspekta Samwel.

Kwa nukta hiyo anasimama wakili Magafu na kuendelea kumhoji shahidi.

Wakili Magafu: Una exhibit page 9 (kielelezo namba tisa)?

Shahidi: Ndiyo ninayo.

Wakili Magafu: Tafuta sehemu yoyote ile imeandikwa mshtakiwa anasema yuko tayari kutoa maelezo ya ungamo mbele yako?

Shahidi: Specifically hakuna.

Wakili Magafu: Ulimuuliza mshtakiwa nini maana ya mlinzi wa amani?

Shahidi: Hapana.

Wakili Magafu: Jina lako la mwisho ni nani?

Shahidi: Cloud.

Wakili Magafu: Utakubaliana na mimi hayo majina yanatumika na kila mtu?

Shahidi: Ndiyo.

Wakili Magafu: Gari ya DFP unajua maana yake?

Shahidi: Ndiyo, maana yake ni Donors Project Fund.

Wakili Magafu: Ni kweli gari ambazo zimesajiliwa kwa DFP ziko nyingi hapa mjini?

Shahidi: Ni kweli zipo.

Wakili Magafu: Gari ambazo zinatumika na polisi zina namba gani?

Shahidi: PT

Wakili Magafu: Utakubaliana na mimi kuwa ukiandika maelezo unatakiwa uwe makini sana?

Shahidi: Nakubali.

Wakili Magafu: Kwanini hukujielekeza kwenye upungufu uliotokea kwenye ile karatasi ya maungamo?

Shahidi: Ni makosa ya kibinadamu.

Wakili Magafu: Ni utaratibu gani unapotakiwa kusainisha karatasi zenye kurasa zaidi ya mbili au moja?

Shahidi: Kusaini karatasi ya kwanza hadi ya mwisho.

Wakili Magafu: Ni kwanini kuna umuhimu kila ukurasa muweke saini wote,na kwa ajili ya ku prevent (kuzuia) nini?

Shahidi: Ili mmoja asije akamgeuka mwenzake.

Wakili Magafu: Ulilifanya hilo?

Shahidi: Sikufanya hilo.

Wakili Magafu: Ni kwamba ndiyo maana mshtakiwa anasema hizo karatasi nyingine hazijui utasemaje?

Shahidi: Hiyo karatasi naiamini kuwa ni salama, asiikane.

Wakili Magafu: Wewe umeona hayo yote yaliyotokea siyo upungufu?

Shahidi: Kwangu mimi siyo upungufu.

Wakili Magafu: Ni nani alikuwa hakimu mkuu mahakama ya mwanzo?

Shahidi: Sijui.

Wakili Magafu: Baada ya kuandika maelezo hayo ya mshtakiwa ulisaini bila taratibu za sheria kufuatwa?

Shahidi: Siyo kweli.

Wakili Magafu: Uliwahi kumuuliza mshtakiwa kuwa yeye na marehemu (Msuya) walikuwa na ugomvi gani?

Shahidi: Sikuwahi kumuuliza.

Wakili Magafu: Uliwahi kumuuliza wenzake aliowataja kama walikua na ugomvi na marehemu?

Shahidi: Sikuwahi kumuuliza.