Mashahidi wakwamisha kesi ya bilionea Msuya

Watuhumiwa saba wa kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Erasto Msuya, wakielekea katika chumba cha Mahakama Kuu Kanda ya Moshi kwa ajili ya kusikiliza kesi inayowakabili.Picha na Dioinis Nyato

Muktasari:

  • Akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo, wakili mwandamizi wa Serikali, Peter Maugo, alidai kuwa taarifa walizonazo mmoja wa mashahidi hao amelazwa kwa matibabu.

Moshi. Udhuru wa mashahidi wawili waliotarajiwa kutoa ushahidi katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara tajiri wa Mirerani, Erasto Msuya, jana ulisababisha kesi hiyo kuahirishwa hadi leo.

Akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo, wakili mwandamizi wa Serikali, Peter Maugo, alidai kuwa taarifa walizonazo mmoja wa mashahidi hao amelazwa kwa matibabu.

Chavula alidai taarifa waliyopewa na mkuu wa upelelezi (RCO) Mkoa Kilimanjaro, mbali na shahidi huyo kulazwa, mwingine alichelewa kupata wito wa mahakama wa kufika kortini hiyo jana.

“Huyu ambaye wito ulichelewa kumfikia kwa sasa ni mkazi wa nje ya Mkoa Kilimanjaro na tunavyozungumza sasa hivi yuko kwenye maandalizi ya kuja kesho (leo) kutoa ushahidi,” alieleza.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, wakili John Lundu, alidai kwa mazingira yaliyoelezwa na upande wa mashtaka, wao hawana pingamizi kwa Mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi leo.

Jaji Maghimbi aliulizia afya ya shahidi mwingine aliyekuwa atoe ushahidi wake juzi, mrakibu mwandamizi wa polisi (SSP), Vincent Lyimo, inavyoendelea na kama ataweza kufika kortini leo.

Juzi, wakili wa Serikali mkuu, Peter Maugo alimweleza Jaji kuwa ingawa shahidi huyo, SSP Lyimo, alikuwa tayari kutoa ushahidi wake ni vyema akaruhusiwa kuondoka hadi siku nyingine.

Wakati wakili huyo akitoa maelezo hayo, shahidi huyo alikuwa amesimama mbele ya Jaji, huku mkono wake wa kulia ukiwa na kifaa maalumu (canula) cha kupitisha dawa kwenda kwenye mishipa ya damu.

“Tungeiomba mahakama imruhusu na kumpa siku nyingine ingawa amesema yuko tayari kutoa ushahidi wake, lakini kwa tatizo hilo la afya aweze kutoa keshokutwa (Alhamisi),” alieleza Maugo.

Jaji Maghimbi alikubali ombi hilo na kumuonya shahidi huyo kuwa awepo kwa vile tayari kumbukumbu za Mahakama za kesi hiyo, zimeshaingia kuwa atatoa ushahidi siku ya leo.

Kwa siku ya jana, Jaji Maghimbi alisisitiza uwapo wa shahidi huyo na wakili Chavula akamweleza kuwa, baada ya mahakama kuahirishwa wangefuatilia kujua maendeleo ya afya yake.

Msuya aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa ndani na nje ya Arusha, aliuawa kwa kwa kutumia bunduki ya kivita ya Sub Machine Gun (SMG) Agosti 7, 2013 katika eneo la Mijohoroni wilayani Hai.