Mashahidi wanne wammaliza Scorpion ahukumiwa miaka saba jela

ALIYETOBOLEWA MACHO NA SCORPION ALONGA BAADA YA HUKUMU

Muktasari:

Aliyetobolewa macho ashangazwa na adhabu, aomba kuonana na Rais Magufuli

Dar es Salaam. Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Ilala, Flora Haule amemuhukumu Salum Njwete, maarufu kwa jina la Scopion, kwenda jela kwa miaka saba na kulipa haraka fidia ya Sh30 milioni baada ya kuridhika na maelezo ya mashahidi wanne uliodhihirisha kuwa mshtakiwa alimjeruhi Said Mrisho kwa kumtoboa macho yote.

Hata hivyo, Hakimu Haule amesema ushahidi wa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kuwa mshtakiwa alifanya kosa la unyang’anyi kwa kutumia silaha.

Lakini Mrisho amesema hajaridhika na hukumu hiyo, akisema haiendani na kosa alilotenda mshtakiwa kwa kuwa amemuacha akiwa kipofu na tegemezi.

“Sijajua utaratibu wa kulipwa hizo hela. Kwanza Sh30 millioni ni hela ndogo sana,” alisema Mrisho baada ya hukumu hiyo.

“Nitaomba kuonana na Rais (John Magufuli) kwa kuwa sina uwezo wa kufanya shughuli yoyote. Hata watoto wangu nimewahamisha shule kutokana na kukosa ada.”

Kutokana na tukio hilo kuripotiwa na vyombo vya habari, Mrisho alipata misaada kutoka kwa watu walioguswa, ikiwa ni pamoja na pikipiki za magurudumu matatu kwa ajili ya kufanyia biashara.

Scorpion anadaiwa kutenda kosa hilo Septemba 6, 2016 saa 4:00 usiku, maeneo ya Buguruni. Anadaiwa kumchoma Mrisho sehemu mbalimbali za mwili ikiwamo machoni, tumboni na mabegani akitumia kitu chenye ncha kali.

Pia anatuhumiwa kuiba vitu vyenye thamani ya zaidi ya Sh300,000.

Ushahidi uliomtia hatiani

Hakimu Haule alisema ushahidi uliotolewa na shahidi wa saba na wa nane katika kesi hiyo, umeonyesha kuwa Njwete alikuwa mlinzi katika eneo la wafanyabiashara wa Buguruni na alikuwa na jukumu la kuhakikisha vibaka wanapungua eneo hilo.

Haule alisema shahidi wa kwanza ambaye ni Mrisho ameonyesha jeraha la macho alilolipata.

Pia, alisema wakati tukio hilo linatokea, jina la Njwete lilikuwa likitajwa na baadhi ya wafanyabiashara, jambo linalofanya ushahidi huo kutotia shaka.

Alisema matokeo ya uchunguzi uliofanywa na shahidi wa nne na wa tano ambao wote ni madaktari kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) umethibitisha kuwa Mrisho alichomwa na kitu chenye ncha kali machoni na kusababisha asiweze kuona tena.

Lakini hakukubaliana na hoja ya uporaji wa kutumia silaha.

“Nimepitia hoja zote za upande wa mashtaka wameshindwa kuthibitisha kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha. Mahakama imeona nia ya mtuhumiwa ilikuwa kupambana na vibaka,” alisema Haule.

Baada ya Hakimu Haule kutoa maelezo hayo, wakili wa Serikali, Frank Tawali aliomba mahakama itoe adhabu stahiki kwa kuwa Mrisho amekuwa tegemezi, pia Taifa limepoteza nguvu kazi kwa kuwa amekuwa kipofu.

Lakini wakili wa utetezi, Hussein Hitu aliiomba mahakama kumpunguzia mteja wake adhabu kwa sababu ameshakaa ndani kwa muda mrefu na ana familia inayomtegemea.

Haule alitoa hukumu hiyo kutumikia kifungo cha miaka saba jela na kulipa fidia ya Sh30 milioni itakayotakiwa kulipwa haraka.

Awali, Oktoba 19, 2017 Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) aliomba kutoendelea na kesi hiyo kutokana na mapungufu kwenye mashtaka, lakini akafungua upya kesi hiyo baada ya kurekebisha mashtaka ya awali.

Kesi hiyo ilirudi mahakamani Novemba 30, 2017 wakati mshtakiwa aliposomewa mashtaka upya.