Mashindano ya Urembo yalivyofungua nyota ya Maua Sama

Maua Sama

Muktasari:

Maua anasema wakati akiwa shule alitoroka na kwenda Jijini Dar es Salaam kwa siri kwenda studio, japokuwa alikuwa akimuaga mama yake ambaye alificha siri baba yake asijue.

Ukiwataja wasanii kumi wa kike wanaofanya vizuri katika soko la muziki hapa Bongo, Maua Sama huwezi kuacha kutaja jina lake.

Msanii huyu anayefanya muziki wa taratibu, kipaji chake kilianza kujulikana aliposhiriki mashindano ya urembo katika Chuo Kikuu cha Ushirika kilichopo Moshi, Kilimanjaro.

Maua ambaye ametesa na vibao vikali ikiwemo Mahaba Niue, Sisikii vilivyomtambulisha vyema kwenye soko la muziki, anasema pamoja na kushiriki mashindano hayo ya urembo sio fani aliyoizimikia.

Anaeleza kwamba anashukuru kwa ushauri wa marafiki zake kutaka aingie katika mashindano hayo imekuwa njia ya kuonyesha kipaji cha kuimba ambacho alikuwa nacho tangu akiwa mdogo.

Anasema pamoja na kuwa mshindi wa pili katika mashindano hayo ya urembo yaliyofanyika miaka nane iliyopita chuoni hapo akiwa anasoma ngazi ya cheti, kati ya vitu alivyowakimbiza ni kipengele cha vipaji ambapo hakuna aliyekuwa akimfikia katika kuimba.

Hata hivyo anasema katika kufanikisha ndoto hizo, dada wa mmoja wa rafiki zake alimkubali alipomuona akimba na kuamua kumuunganisha na msanii wa siku nyingi MwanaFA ambaye alikuwa na ukaribu naye.

“Kwa kuwa nilikuwa Moshi nilikuwa nikimrushia Mwana FA nyimbo ambazo nimeimba na baada ya kuzisikiliza na kukubali kipaji changu aliniita Dar es Salaam niende nikafanye naye kazi na katika hizo nyimbo ya kwanza tuliitoa ilikwenda kwa jina la ‘So Crazy,” anasema Maua.

Hata hivyo, kutokana na kutojua mambo mengi katika muziki, anasema Mwana FA aliamua kumpelekea Jumba la Kukuza Vipaji (THT), kwa ajili kuusoma vizuri muziki.

Akiwa THT ilipofika mwaka 2016 akaachia kibao cha ‘Sisikii’, 2017 akaendeleza makali yake kwa kuachia Mahaba Niuwe na kuzidi kumuweka katika nafasi ya wasanii wa kike wanaofanya vizuri hapa nchini.

Aliwezaje kufanya muziki na shule

Maua anasema wakati akiwa shule alitoroka na kwenda Jijini Dar es Salaam kwa siri kwenda studio, japokuwa alikuwa akimuaga mama yake ambaye alificha siri baba yake asijue.

Lakini kadri alivyokuwa akifanya vizuri alisikika kwenye vyombo vya habari, huku baadhi ya watu waliokuwa wakifanya kazi na baba yake wakiwa wanampa hongera.

Anasema kwa kuwa baba yake hakuwa mtu wa kusikiliza muziki, alikawia kujua mpaka pale aliposikilizwa nyimbo na baadhi ya wafanyakazi wenzake chuo cha Ushirika, ambapo alikuwa akifundisha hapo na mwisho wa siku kumkubalia aendelee.

Hata hivyo baada ya kumaliza shule ngazi ya Shahada, Mwana FA alimuombea ruhusa kwa baba yake aende akaishi Dar es Salaam kwa ajili ya kujitanua zaidi kimuziki.

“Nashukuru baada ya kwenda Dar es Salaam niliishi kwa rafiki yangu huku naenda THT mpaka pale nilipoiva kisanii na kuweza kusimama na kuwa na kwangu,” anasema Maua.