Mashirika 47 kutoa gawio kwa Serikali

Muktasari:

  • Taarifa iliyotolewa leo Julai 22, 2018 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa imesema shughuli hiyo itafanyikia katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam

Dar es Salaam. Wakala, Kampuni, Taasisi na Mashirika ya Umma 47 ambayo Serikali inamiliki hisa, kesho Julai 23, 2018 yatakabidhi gawio la mwaka 2017/18 kwa Rais John Magufuli.

Taarifa iliyotolewa leo Julai 22, 2018 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa imesema shughuli hiyo itafanyikia katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Msigwa amesema kabla ya shughuli hiyo, Rais Magufuli na Waziri Mkuu wa Korea Kusini, Lee Nak-Yon watashuhudia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa daraja jipya la Selander la jijini Dar es Salaam na njia zake.

Amesema hafla ya utiaji huo wa saini itafanyikia Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) itatiliana saini na mkandarasi aliyeshinda zabuni ya ujenzi wa daraja hilo.

Msigwa amesema daraja la Selander litaunganisha eneo la Agha Khan katika barabara ya Barack Obama na eneo la Coco Beach katika makutano ya barabara za Kenyatta na Toure.