Wednesday, January 11, 2017

Maskini! Mama aua kichanga kwa kukitupa ziwani

 

By Ngollo John, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Mwanza. Polisi mkoani Mwanza inamshikilia mwanamke kwa kosa la kutupa mtoto wake ziwani.

Mwanamke huyo mkazi wa Butuja wilayani Nyamagana anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumtupa mtoto mchanga wa kiume wa siku moja ndani ya Ziwa Victoria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amesema mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Januari 9, saa kumi jioni katika Kata ya Pasiansi wilayani Ilemela.

Amesema wakazi wa eneo hilo walibaini maiti ya kichanga hicho na kutoa taarifa polisi ambao walifanya uchunguzi na kumbaini mtuhumiwa ambaye alikiri kutenda kosa hilo.

Katika tukio jingine, kamanda huyo amesema mtembea kwa miguu ambaye hajafahamika jina lake anayekadiriwa kuwa na miaka 50,  amekufa papo hapo baada ya kugongwa na gari aina ya Toyota Hilux.

Amesema ajali hiyo ilitokea katika eneo la  Usagara wilayani Misungwi na kwamba, polisi wanamshikilia

dereva wa gari hilo kwa mahojiano zaidi.

 

-->