VIDEO-Baba mzazi asimulia siku za mwisho za Masogange

Muktasari:

  • Baba yake asema kabla ya kwenda Dar es Salaam walikosana

 Gerald Waya, ambaye ni baba mzazi wa Agnes (Masogange), amesema mwanaye alikuwa nguzo katika maisha yake, hivyo ni pigo kubwa kwake na familia nzima.

Waya akizungumza na MCL Digital nyumbani kwake Mbalizi II wilayani Mbeya, leo Aprili 22, 2018 amesema Masogange ni mtoto wanne katika familia yake ya watoto sita, wa kike wakiwa watano.

Amesema Masogange alisoma Shule ya Msingi Utengule-Mbalizi na sekondari ya Sangu alikoishia kidato cha pili.

Waya amesema Masogange alipata matatizo hivyo akalazimika kuacha shule. Hata hivyo amesema hataki kuzungumzia mambo mabaya wakati huu anapoomboleza kifo cha mwanaye.

 “Aliishia form two (kidato cha pili), akapata matatizo ikabidi aache shule. Tulikosana kidogo lakini tukayamaliza yeye akaenda Dar es Salaam,” amesema.

Waya amesema, “Mwanangu alikuwa nguvu kwangu, alikarabati nyumba hii ninayoishi kwa sasa na nilikuwa nafarijika sana, lakini leo kusikia msiba huu kwa kweli inaniuma sana.”

Amesema Masogange alimpigia simu, “Tukaongea naye akaniambia ‘mimi baba ninaumwa’. Nikamuuliza nini tatizo akasema, “aah!   baba niombee tu kwa Mungu’. Na Jumamosi iliyopita nilimpigia simu wakati yupo hospitali kujua maendeleo yake lakini akaniambia ‘baba byee’.  Nikaanza kulia, na hapo sikuwasiliana naye tena hadi nilipopata taarifa za kifo chake,” amesema.