Maswali manne ya Kamanda wa Polisi kutekwa kwa Mo Dewji Tanzania

Muktasari:

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ameeleza mambo manne anayojiuliza kufuatia tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’


Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amehoji maswali manne kufuatia tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’.

Mfanyabiashara huyo alitekwa jana alfajiri Oktoba 11, 2018 jijini Dar es Salaam kwenye Hoteli ya Colosseum iliyopo Oysterbay alipokwenda kwa lengo la kufanya mazoezi.

MCL Digital imezungumza na Mambosasa jana Alhamisi Oktoba 11, 2018  na kubainisha kuwa kuna maswali yamekuwa yakiwasumbua, ambayo wanatafuta majibu yake na kuyakosa.

Swali la kwanza

“Hebu tujiulize kamera (iliyopo katika hoteli ya Colosseum) nayo imeshindwa kutupatia kila kitu kuna upande tumeshindwa kuupata vizuri tunajiuliza ilikwepeshwa makusudi?” amehoji Mambosasa.

Swali la pili

Mambosasa amesema watekaji walifika mapema kabla ya MO lakini walikuwa hapo hapo hotelini, kushangazwa na walinzi kutowachukulia hatua ikiwa ni pamoja na kutowauliza sababu za kutoshuka kwenye gari walilokuwa wamepanda.

Swali la tatu

“Tatu tunaambiwa wakati zoezi linafanyika hakukupigwa yowe wala majibizano ya risasi ina maana hawa waliokuwa hapa walilichukuliaje tukio hili?” amehoji.

Swali la nne

Katika swali lake la nne Mambosasa amesema hakuna aliyeandika gari zinazoingia katika hoteli hiyo, “kwahiyo hebu tufanye uchunguzi.”

Soma zaidi