VIDEO-Maswali matano yaibuka kutekwa mwanafunzi UDSM

Muktasari:

Wanasema maelezo yaliyotolewa na polisi hayajaweka wazi baadhi ya mambo hivyo kuibua maswali zaidi kuhusu kutoweka kwa mwanafunzi huyo anayeshikiliwa na Kanda Maalumu ya Kipolisi Dar es Salaam.

Wanasheria na wanaharakati wameibua maswali matano kuhusu sakata la mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo, anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa siku 10 sasa kwa madai ya kudanganya kuwa alitekwa.

Wanasema maelezo yaliyotolewa na polisi hayajaweka wazi baadhi ya mambo hivyo kuibua maswali zaidi kuhusu kutoweka kwa mwanafunzi huyo anayeshikiliwa na Kanda Maalumu ya Kipolisi Dar es Salaam.

Nondo, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), alidaiwa kutoweka usiku wa kuamkia Machi 6 na kupatikana usiku wa Machi 7 huko Mafinga, Iringa baada ya kudaiwa kujisalimisha polisi.

Swali la kwanza linaloibuka ni kwa nini polisi hawamuweki wazi mpenzi wa Nondo na kumhoji kama walivyoeleza awali kuwa walifuatilia mawasiliano ya mwanafunzi huyo na kubaini alikwenda Mafinga kwa mpenzi wake.

Pia wamehoji sababu za Jeshi la Polisi Iringa na Dar es Salaam kutoa kauli zinazokinzana kuhusu tukio hilo.

Tatu, ni suala la mwanafunzi huyo kutopewa dhamana wala kufikishwa mahakamani; nne, sababu zilizotolewa na polisi kwamba hakutekwa kwa kuwa hakuwa na jeraha lolote wala mchubuko na tano ni taarifa za uchunguzi kwa watu mbalimbali waliotekwa kutowekwa wazi.

Kupewa dhamana

Wakili wa mwanafunzi huyo, Jebra Kambole alisema mteja wao anashikiliwa na polisi kinyume cha sheria kwa maelezo kuwa tangu akamatwe zimeshapita saa 24 ambazo zinairuhusu polisi kuwa naye kwa mujibu wa kifungu cha 20 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai namba 32 (1).

Kambole alisema wanashangaa kuona Nondo anashikiliwa zaidi ya wiki sasa, huku ikionekana hakuna dalili za kupewa dhamana wakati kosa lake lina dhamana.

“Tumewasiliana na polisi mara kadhaa ili watukutanishe na mteja wetu lakini wametukatalia wakitueleza kwamba wamemshikilia kama mwathirika na sio mtuhumiwa, hivyo watatuita pale watakapokuwa wanamuhoji kama mtuhumiwa,” alisema Kombole.

“Kwa hali ilivyo tumeamua kufungua kesi Mahakama Kuu ili iweze kutusaidia kuamuru polisi wamfikishe mahakamani ambapo tutajua anashikiliwa kwa makosa gani kwa sababu Mahakama ina mamlaka kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Madai ya kwenda kwa mpenzi wake

Kombole alisema taarifa ambayo inatolewa na polisi kuwa Nondo alikwenda kwa mpenzi wake Mafinga, haipaswi kuaminiwa kwa sasa kwa kuwa mteja wao hakupewa nafasi ya kuzungumza na mawakili wake kubainisha nini kilichomkuta, kwamba mpaka sasa bado hawajazungumza naye jambo lolote.

Kauli polisi Iringa, Dar kupishana

Machi 8, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire alisema Nondo alijisalimisha polisi na kudai alitekwa na watu ambao walimtelekeza, kwamba wamefungua jalada la uchunguzi ili kubaini iwapo alitekwa au alitoa taarifa za uongo kwa lengo la kuhamamisha wanafunzi kuvuruga amani.

Wakati Bwire akieleza hayo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema mwanafunzi huyo alionekana Mafinga akiendelea na shughuli zake na wala hakuripoti tukio la kutekwa kituo chochote cha polisi na kwamba ndio sababu ya kuendelea kumshikilia.

Akizungumzia kupishana kwa kauli hizo Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Gaudence Mpangala alisema kauli zilizotolewa na makamanda hao zinapishana huku zikionyesha kulenga kuunga mkono viongozi wa Serikali aliodai kuwa kabla ya uchunguzi wa polisi kukamilika, waliibuka na kudai kuwa Nondo amejiteka, anapaswa kuchukuliwa hatua kali.

“Kauli zao zinawaumbua inaonyesha wanafanya kazi ili kuunga mkono kauli za baadhi ya viongozi waliozungumzia tukio hilo hata kabla uchunguzi kukamilika,” alisema Profesa.

Profesa Mpangala alisema matukio ya baadhi ya watu kutekwa, kuteswa na kuuawa yapo, hivyo Polisi kuunganisha tuhuma za mwanafunzi huyo kujiteka huku wakiahidi kuendelea na uchunguzi ni mambo yanayoshangaza.

Kutokutwa na majeraha

Wakili Faraji Mangula alisema kwa mujibu wa sheria si lazima mtu aliyetekwa awe amejeruhiwa, anaweza asiwe na vyote hivyo lakini akatambuliwa kwa kuathirika kisaikolojia.

Mangula ametoa kauli hiyo baada ya Mambosasa kusema Nondo alikuwa na afya njema, hakupewa dawa yoyote ya kumlevya na hakuwa na majeraha.

Katika ufafanuzi wake Mangula alisema mtu aliyetekwa anaweza kutambulika kwa vitu vingi ikiwamo makovu yanaonyesha alipata kipigo au majeraha mabichi au kuathirika kisaikolojia.

Taarifa za uchunguzi

Mangula aligusia taarifa za uchunguzi wa matukio ya utekaji kutoanikwa hadharani, “Sheria ina upungufu kwenye masuala ya uchunguzi, ikilinganishwa na nchi nyingine ambazo taasisi au watu binafsi huchunguza. Hapa kwetu polisi pekee ndiyo wanachunguza, hata kama wenyewe ndiyo watuhumiwa.”

Alibainisha kuwa anayepaswa kuwahoji polisi kwa utendaji wao ni Mkuu wa Jeshi la Polisi au Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora ambayo ilianzishwa kwa lengo hilo.

Alisema taasisi hizo mbili zinapochelewa kushughulikia mambo hayo, ndipo jamii inashuhudia taasisi hiyo ikishikilia watu kinyume cha sheria, au kuchunguza baadhi ya matukio katika hali ambayo inaacha maswali mengi kwa jamii.

Kwa nini polisi wanatamka kwamba amesingizia kutekwa wakati yeye mwenyewe hajawahi kutamka kwamba ametekwa ila aliandika kwenye kupitia simu yake kwamba , “I am at high risk.”