Maswali tata kauli za Kamanda Sirro

Muktasari:

Kutoweka kwake na mkutano wa mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro bado vinaacha maswali ambayo wananchi wanajiuliza. 

Mwandishi Wetu, Mwananchi
[email protected]

Dar es Salaam. Maelezo ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro juu ya waliyogundua hadi jana kuhusiana na kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’ yameibua upya maswali na utata wa suala hilo.

Sirro aliitisha mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana ili kueleza maendeleo ya uchunguzi wa utekeji huo ambao umeleta taharuki kubwa miongoni mwa wananchi, wanasiasa na wafanyabiashara.

Baada ya mkutano huo, mjadala mkubwa ulizuka kwenye mitandao ya kijamii na kwingineko huku wanaharakati, wanasiasa na wananchi kwa ujumla wakihoji masuala kadhaa kuhusu maelezo ya Sirro katika tukio hilo.

Mo Dewji (43) alitekwa saa 11:30 alfajiri ya Oktoba 11 katika Hoteli ya Colosseum, Oysterbay jijini Dar es Salaam na watu ambao polisi ilidai ni Wazungu wawili waliotumia gari aina ya Toyota Surf.

Tangu siku hiyo, hakuna taarifa yoyote kutoka mamlaka za upelelezi yenye kutia matumaini ya kupatikana kwa mfanyabiashara huyo , huku familia yake ikitangaza dau la Sh1 bilioni kwa atakayetoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa ndugu yao.

Kwa nini picha za CCTV hazikutolewa mapema?

Katika mkutano wa jana, IGP Sirro alisema kamera za usalama (CCTV) katika hoteli aliyotekwa Dewji na nje ya hoteli, zimewasaidia kulitambua gari lililotumika kwenye uhalifu dhidi yake.

“Kwenye CCTV kuanzia Colosseum inaonyesha limepita barabara ya Ali Hassan Mwinyi na kuendelea hadi kwenye roundabout (mzunguko) ya Kawe. Bado tunaendelea kufuatilia kama walielekea upande wa Silver Sands (White Sands?) au Kawe,” alisema Sirro.

Wadadisi wanahoji ni kwa nini jeshi la polisi halikutoa picha za gari au tukio hilo kwenye vyombo vya habari muda mfupi baada ya tukio ili wananchi walitambue na kutoa taarifa.

“Polisi wamekuwa mstari wa mbele kuomba wananchi tuwasaidie kwa taarifa za uhalifu, kwa nini hawakutoa hizo picha muda mfupi baada ya tukio kama wanavyofanya nchi nyingine ili tusaidie?,” alihoji mkazi mmoja wa Msasani.

Maswali yameulizwa pia kuhusu mwonekano wa picha za gari hilo zilizoonyeshwa na Kamanda Sirro jana kwamba zilipigwa kutoka wapi. Picha hazionyeshi kuwa zilipigwa kutoka juu ambako CCTV mara nyingi huwekwa. Wengine wanahoji pia kwanini polisi wameshindwa kutoa picha za video ambazo zingekuwa msaada zaidi.

Picha ya dereva

Jana Sirro alisema kwa kushirikiana na Polisi wa Interpol, wamefanikiwa kujua nchi lilipotoka gari lililotumika kwenye utekaji wa Dewji lilitoka nchi jirani na dereva aliyekuwa akiliendesha aliyemtaja kwa jina la Obasanjo Zacharia Junior. “Na watu wetu watazunguka hizo nchi kuona tunawapata,” alisema Sirro.

Kufuatia kauli hiyo, wachambuzi wanahoji kwa nini polisi hawajatoa picha za dereva huyo hadharani ili raia wema wanaomjua watoe taarifa wakimwoma kama kweli wanamjua mwenye gari na dereva aliyekuwa akiliendesha.

Hata hivyo, jana Sirro alisisitiza kuwa taarifa nyingine zote kuhusiana na picha na mpaka lilikopita gari hilo ni za kiuchunguzi na haitakuwa busara kuzitoa sasa.

Sirro apishana na Mambosasa

Saa chache baada ya tukio la kutekwa kwa Dewji, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema kamera za usalama katika hoteli ya Colosseum zilishindwa kutoa mtiririko mzima wa tukio kwa sababu zilisoma upande mmoja.

“Bado tunaendelea na upelelezi, dada (mwandishi) kama kitu hakionekani huwezi kumuona mtu, huwezi kujua gari ni ya aina gani, ndicho kitu ambacho hatujakiona…kamera hazisomi,” alisema Kamanda Mambosasa alipoulizwa na mwandishi wiki iliyopita.

Hata hivyo, jana IGP Sirro alisema picha za gari wanaloamini lilitumika katika utekaji huo zilichukuliwa katika kamera zilizofungwa kwenye hoteli ya Colosseum na kuleta mgongano wa kauli kati ya vigogo hao wa polisi.

Jambo jingine, watu wengine wanahoji kuwa maelezo ya Mambosasa alisema gari mbili zilitumika katika utekaji huo, mbona ni gari moja tu linaonyeshwa. Vipi lile gari lililotoa ishara?

Wachunguzi kutoka nje

Kauli nyingine ya Sirro iliyokaribisha maswali mengi ni pale aliporudia msimamo wa Serikali kuwa haitaruhusu wachunguzi kutoka nje kwa sasa kwa kuwa wana uwezo wa kutosha kuchunguza tukio hilo kama walivyopingwa

“Suala la nani aje kutusaidia sisi vyombo vya dola ndiyo tunaweza kuona sababu ya kufanya hivyo. Kwa hali tuliyonayo sidhani kwamba tunahitaji watu wa kutusaidia. Ni lazima tuendelee kulinda heshima ya nchi yetu,” alisema Sirro.

Msimamo huo wa Sirro ulikumbana na maswali mengi. “Kama ni hivyo kwa nini tumetunga sheria ya kusaidiana katika masuala ya kijinai. Kama tunajitosheleza katika masuala hayo kwa nini bado tunapeleka polisi wetu nchi za nje kama Marekani kujifunza? alihoji Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Ni gari kutoka Msumbiji?

Namba za gari linalosadikiwa kutumika katika kumteka Dewji zilizoonyeshwa na Sirro jana, zimeibua pia maswali, gari hilo ni la nchi gani. Namba hizo zinasomeka AGX 404 MC.

Ingawa Sirro hakutaka kutoa maelezo zaidi kuhusu utambulisho wa gari hilo kwa sababu za kiupelelezi, kibao na namba za gari hilo vinafanana kabisa na vile vinavyotumika nchi jirani ya Msumbiji.