Maswali ya mwaka mpya kwa Freeman Mbowe

MBOWE AFICHUA MIKAKATI YA CHADEMA 2018

Muktasari:

Katika kufunga mwaka 2017, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe Jumapili iliyopita alikutana na wanahabari kutoa salamu za na mwelekeo wa chama hicho kwa mwaka 2018 nyumbani kwake Dar es Salaam.

Katika kufunga mwaka 2017, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe Jumapili iliyopita alikutana na wanahabari kutoa salamu za na mwelekeo wa chama hicho kwa mwaka 2018 nyumbani kwake Dar es Salaam. Yafuatayo ni baadhi ya maswali na majibu yaliyoulizwa na wanahabari na majibu yake. Endelea

Swali: Dhana ya utawala bora ni pamoja na matumizi sahihi ya fedha za Serikali, wewe kama Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni unaridhika na namna matumizi ya fedha za Serikali yanavyofanyika?

Jibu: Hili ni tatizo kubwa ambalo lipo na linaendelea kuwapo. Fedha za Serikali zinatakiwa kutumika baada ya kupitishwa katika Bajeti. Hakuna fedha yoyote ambayo inatakiwa kutumika bila kupitishwa katika utaratibu wa kijabeti, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba hivi sasa fedha zinatumika nje ya mfumo wa Bajeti. Mimi na wenzangu haturidhiki na utaratibu huu unaoendelea na tumelilalamikia sana. Fedha zinaelekezwa kwenye miradi mbalimbali bila kupitia utaratibu wa kibajeti kama sheria za manunuzi ya umma zinavyotaka.

Ndege za serikali zimenunuliwa nje ya mfumo wa kibajeti, hivi sasa si ajabu kumsikia rais akielekeza mahakama ipewe kiasi fulani cha fedha, si jambo baya kukisaidia chombo hicho cha kutafsiri sheria, lakini utaratibu huu ni kwenda kinyume na sheria pamoja na utawala bora. Umefika wakati wa kuanza kuheshimu sheria zetu hasa zinazohusu matumizi ya fedha za Serikali, tutumie utaratibu unaoruhusiwa kisheria wa kibunge wa kutumia fedha za Serikali.

Swali: Umesema Mwaka 2017 haukuwa mzuri kwa Chadema katika kufanya siasa. Chadema imepata misukosuko mingi na imekuwa na kesi nyingi, tueleze tathimini yenu kesi hizi zimegharimu kiasi gani.

Jibu: Ni kweli mwaka 2017 haukuwa mzuri kwetu kisiasa lakini si kwa Chadema tu bali ni taifa kwa ujumla kwa sababu Chadema wakinyimwa haki madhara yake yanakwenda kwa watu wengi zaidi.

Ni kweli tuna kesi nyingi za kubambikiwa ambazo ziko kwenye mahakama zote za mikoa, wilaya na hata kwenye kata tuna kesi nyingi, ziko kesi katika kila mkoa, wilaya na hata kata. Katika kuendesha kesi hizi ni gharama kubwa siyo za fedha tu bali hata gharama za muda. Viongozi wetu na wanasheria wanatumia muda mwingi kushughulikia kesi hizo ingawa siwezi kukadiria gharama za kesi hizi lakini ni gharama kubwa sana.

Swali: Katika salamu zako hukuzungumzia hali ya Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu ambaye alipigwa risasi na hili ni tukio kubwa la mwaka huu.

Jibu: Tundu Lissu ameimarika na sasa anaweza kusimama, kukaa, tangu amepigwa risasi hajawahi kukaa mwenyewe bila kukalishwa, lakini juzi ameweza kukaa, mwenyewe anatembea ingawa kwa taabu. Kimsingi matibabu amemaliza sasa hivi hapewi dawa zozote bali anafanyiwa mazoezi. Gharama za matibabu hadi sasa zimefikia Dola za Marekani 300,000 inakaribia kwenye bilioni na gharama zitaendelea. Niwashukuru Watanzania waliosaidia Lissu. Serikali na Bunge hawajatoa chochote ingawa waliahidi, kazi kubwa iliyofanywa na Hospitali ya Nairobi kimsingi imekamilika.

Jumamosi Januari 6 2018 ataondoka katika Hospitali ya Nairobi na kupelekwa katika nchi mojawapo ya Ulaya kwa ajili ya tiba ya mazoezi ingawa kwa sasa siwezi kuwatajia nchi anayoenda kwa sababu za kiusalama. Baadaye akishafika tutawatajia nchi hiyo.

Swali: Tumesikia Lissu bado amebaki na risasi moja mwilini, unasemaje kuhusu hilo.

Jibu: Hilo ni suala binafsi ambalo siwezi kulizungumzia lakini ninachofahamu kwa mtu yeyote risasi inaweza kubaki mwilini na isilete madhara mwilini na hiyo inategemea na risasi iko sehemu gani ya mwili, lakini hilo ni suala binafsi ambalo siwezi kulizungumzia kwa upande wa Lissu.

Swali: Desemba 31,2017 ilikuwa ni siku ya mwisho kurejesha fomu za rasilimali na madeni kwa Sekretarieti ya Maadili na tumeona Rais amepeleka zake, upande wenu wapinzani mmepeleka fomu hizo?

Jibu: Tumepeleka fomu hizo wabunge wote wamepeleka, mimi nilipeleka kabla hata ya Rais John Magufuli, nilipeleka Desemba 27, 2017 wabunge wa Chadema tulikumbushana tukapeleka. Lakini tunamwomba Rais kwa sababu ya nafasi aliyonayo aonyeshe mfano kwa kuweka hadharani mali anazozimiliki badala ya kujaza fomu na kuwakabidhi sekretarieti. Wananchi wanataka kufahamu viongozi wao wanamiliki mali za aina gani.

Wakati umefika wa kurekebisha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili viongozi wa umma wasiishie tu kujaza fomu za rasilimali na madeni waliyonayo bali yawekwe hadharani ili wananchi wawapime.

Kuna viongozi wengi wa umma, kuna mawaziri, kuna wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya makatibu wakuu, majaji, wabunge, mahakimu lakini sekretarieti ina wafanyakazi wachache wasiozidi 10 ambao hawawezi kuchambua fomu zote za viongozi.

Kinachoonekana ni kwamba kila mwaka viongozi wa umma wanajaza fomu za rasilimali na madeni na fomu hizo zinakwenda kuwekwa kwenye makabati na shughuli inaishia hapo. Ni lazima twende mbali zaidi ya kujaza fomu. Tusijaze fomu kwa mazoea bali tujitathimini tangu tumeanza kuzijaza zimetusaidia nini, mimi mwenyewe nimejaza fomu hizi kwa miaka mingi sasa lakini huwa sielewi nini kinafuata.

Swali: Unaonaje hamahama ya wanasiasa kwenye vyama vya siasa, kuna kiongozi wa umoja wa vijana wa chama chenu amehamia CCM na wabunge wawili ingawa kuna mbunge mwingine amehamia Chadema, nini kauli yako.

Jibu: Hatuna tatizo na wanasiasa kuhama vyama, hiyo ni haki yao, tatizo letu ni sababu wanazozitoa za kuhama vyama. Tatizo letu ni sababu zinazofanana wanazozitoa wakati wa kuhama kama vile wao ni kasuku, wanasema wanampongeza Rais. Hivi kila mbunge anayehama chama anamuungaje mkono rais wakati watu wanalia hali mbaya ya kupanda kwa gharama za maisha. Unamuunga mkono vipi Rais wakati vyombo vya habari vinafungiwa, unamuungaje mkono Rais wakati demokrasia ya vyama vingi inaminywa. Lakini tumewafahamu viongozi ambao wanaweza kuuza uhuru wao kwa vipande vya fedha. Hii imetusaidia kuwapima viongozi wenye roho nyepesi na hata kama wapo wengine wana mipango ya kuhama wahame tu kwa sababu hatuwezi kukaa na wanachama ambao hawana msimamo.

Swali: Mmesusia kushiriki katika chaguzi ndogo zitakazofanyika hivi karibuni. Mtaishia hapo au hata kwenye chaguzi zijazo mtakuwa na msimamo huohuo?

Jibu: Kila jambo na mazingira yake, tulisusia uchaguzi tukitaka tukae katika meza ya mazungumzo kati yetu na wadau wa uchaguzi kama Msajili wa Vyama vya Siasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Jeshi la Polisi ili kujadiliana kuhusu kama maadili ya uchaguzi kama yanafuatwa. Tulisusia baada ya kujadiliana na vyama vitano vya Umoja wa Katiba ya wananchi (Ukawa) kutokana na ukiukaji wa sheria za uchaguzi zilizotokea katika uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika Novemba 2017. Lakini wenzetu wakaona hakuna umuhimu wa kukaa pamoja na sisi ili kujadiliana basi tukaona rafu zilizotokea zitaendelea katika huu tukaamua kujitoa. Huwezi kuingia vitani wakati adui yako anatumia silaha za kemikali ambazo wewe hauna na ukaendelea na vita. Namna mazingira yatakavyokuwa yanabadilika ndivyo nasi tutakavyobadilika.

Swali: Umesema moja ya ajenda ya Chadema katika mwaka 2018 ni upatikanaji Katiba Mpya lakini tunasikia fedha hakuna, azma yetu isipotimia mtafanya nini.

Jibu: Katiba itapatikana ikiwa kuna dhamira ya dhati, suala la fedha hapa halina mashiko, kama tunaona Katiba ni kipaumbele basi itapatikana lakini serikali yetu haina hiki kipaumbele. Ni lazima dhamira ya kupata Katiba mpya ijengwe kwa shinikizo la makundi tofauti wasiachiwe wanasiasa pekee yao. Hii ni katiba ya Tanzania siyo ya vyama vya siasa.

Swali: Kwanini mlisusia uchaguzi badala ya kutumia mikutano ya kampeni kuwasilisha hoja zenu kwa wananchi.

Jibu: Hatuwezi kushiriki katika uchaguzi ambao tunaona mazingira ya ushindani hayako sawa kwa kuwa kila chama kinaposhiriki kwenye uchaguzi lengo lake ni kushinda. Sasa kama uwanja unaonekana kabisa hauko sawa ,hatuwezi kushiriki. Kufikisha hoja kwenye mikutano ya kampeni pekee yake hakutoshi kutuwezesha kushiriki katika chaguzi wakati tunaona hadharani kuna ukiukaji wa sheria.