Matukio ya utekaji yaliyotikisa Tanzania

Muktasari:

Tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji 'Mo Dewji' sil la kwanza kutokea nchini, kuna mfululizo wa matukio kama hayo yaliyotokea miaka ya hivi karibuni likiwemo la mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communication's Limited (MCL), Azory Gwanda ambaye sasa zimesalia siku chache atimize mwaka mmoja tangu achukuliwe na watu wasiojulikana

Dar es Salaam. Kutekwa kwa Mohammed Dewji kunaweza kuwa mfululizo wa matukio kama hayo yaliyotokea miaka ya hivi karibuni.

Wapo waliopatikana wakiwa wazima, wengine walifariki dunia na wengine hawajarejea.

Miongoni mwao ni mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Azory Gwanda ambaye sasa zimesalia siku chache atimize mwaka mmoja tangu achukuliwe na watu wasiojulikana.

Tukio hilo la Novemba 21 mwaka jana lilitokea nyumbani kwake Kibiti mkoani Pwani na hadi  jana alikuwa bado hajapatikana.

Ben Saanane

Mtu mwingine aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha tangu Novemba 28, mwaka jana na hadi jana alikuwa hajarejea ni kada wa Chadema, Ben Saanane. Tukio la kupotea kwa kada huyo ambaye alikuwa msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe liliripotiwa katika kituo cha polisi Tabata jijini Dar es Salaam alikokuwa anaishi na kupewa jalada lenye kumbukumbu namba TBT/RB/8150/2016.

Roma Mkatoliki

Msanii wa Bongo Fleva, Ibrahim Musa maarufu kwa jina la Roma Mkatoliki ni kati ya watu waliotoweka baada ya kudaiwa kutekwa na watu wasiojulikana Aprili 7, mwaka jana.

Kaka wa Roma, Omar Musa alisema ndugu yake alirejeshwa nyumbani saa tisa alfajiri baada ya kutoonekana kwa siku tatu.

Simon Kanguye

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Mkoani Kigoma, Simon Kanguye naye alitoweka na hajulikani alipo tangu Julai 20, mwaka jana akidaiwa kuwa alichukuliwa akiwa ofisini kwake katika jengo la Halmashauri ya Wilaya.

Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Ferdinand Mtui alisema Kanguye alitekwa na watu wasiojulikana.

Samson Josiah

Katika tukio jingine,  mwili wa mmiliki wa mabasi ya Super Sami, Samson Josiah ulikutwa ukielea kwenye Mto Rubana unaotenganisha wilaya za Busega mkoani Simiyu na Bunda mkoani Mara.

Mwili huo ulikutwa ukielea katika mto huo huku ukiwa umefungwa kwenye mfuko wa sandarusi na turubai Machi 14, 2018 saa 10 jioni.

Beuty Yohana

Matukio hayo hayajawaacha salama watoto. Mtoto wa miaka mitatu, Beauty Yohana alipotea baada ya kuchukuliwa na msichana Angel Vincent aliyejifanya ametumwa na mama yake akiwa katika Kanisa la FPCT Mbezi Mwisho, Dar es Salaam.

Tukio hilo la Septemba 22, lilitokea baada ya mama wa mtoto huyo Lucy Maganga kumruhusu binti yake aungane na wenzake katika shule ya Jumapili (Sunday School) wakati mama yake akiendelea na ibada.

Beauty alipatikana Septemba 25, maeneo ya Kivule akiwa mzima wa afya.

 Idrisa Ally

Mtoto Idrisa Ally alipotea Septemba 26 mwaka huu baada ya kuchukuliwa kimafia na mtu asiyejulikana wakati akicheza nyumbani kwao Tegeta Masaiti, jijini Dar es Salaam. Mpaka jana, mtoto huyo alikuwa hajapatikana huku jeshi la polisi likisema linaendelea kumtafuta.

Rehema Juma

Mtoto Rehema Juma mkazi wa Mtaa wa Kingolwira, mkoani Morogoro aliuawa na mwili wake kutupwa kwenye mtaro Kibaha mkoani Pwani baada ya kutekwa na mtu anayedaiwa kuvaa baibui. Tukio hilo la Septemba 12, mwaka jana lilitokea baada ya mtoto huyo kutekwa wakati akicheza jirani na nyumba yao.

Taarifa za tukio hilo ziliibua taharuki kwa wakazi wa mkoa wa Morogoro hasa wenye watoto wadogo. Bibi aliyekuwa anamlea mtoto huyo, Maua Muhongole alisema jitihada za kumtafuta mjukuu wake ziliishia katika kupata taarifa za kupatikana kwa mwili wake Kibaha.

Kibiti, Rufiji na Mkuranga

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), Mei, mwaka huu alimtaka aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kutoa ufafanuzi juu ya kupotea kwa watu akidai kuwa anayo orodha ya kutekwa kwa wakazi 348 wa Mkuranga, Kibiti na Rufiji.