Matukio ya uvamizi ambayo hayajawahi kutolewa majibu

Muktasari:

KAULI

Nimepokea kwa masikitiko tukio la kupigwa risasi Mh. Tundu Lissu, namuombea kwa Mwenyezi Mungu aweze kupona haraka. Aidha vyombo vya dola viwasake wale wote waliohusika na tukio hili la kinyama na kuwafikisha katika mikono ya sheria.

Rais John Magufuli

Dar es Salaam. Tukio la kushambuliwa kwa risasi kwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu limeibua maswali mengi na kukumbusha mengine kama hilo, ambayo uchunguzi wake haujaweza kuwashughulikia wahusika.

Lissu alishambuliwa kwa risasi kati ya 28 na 32 zilizolenga mlango wa abiria wa gari lake aina ya Toyota Land Cruiser alikokuwa amekaa, huku risasi tano zikipiga mwilini.

Inawezekana kukawa na matukio kadhaa yanayoelekea kufanana na hilo, lakini Mwananchi inaangalia matukio mengine sita yanayohusu kutekwa au kushambuliwa kwa watu maarufu, huku wanaofanya vitendo hivyo wakiendelea kuwa “watu wasiojulikana”.

Watu hao maarufu ni pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa jumuiya ya madaktari, Dk Steven Ulimboka; msaidizi wa Freeman Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa Chadema, Ben Saanane; mbunge wa Mtama, Nape Nnauye; mwanamuziki wa kizazi kipya, Roma Mkatoliki; mwandishi wa habari Absalom Kibanda na ofisi za kampuni ya mawakili ya Immma ambayo ililipuliwa usiku.

Kutekwa kwa Dk Ulimboka

Juni, 2012 watu wasiojulikana walimteka Dk Ulimboka na kumpeleka katika msitu wa Mabwepande ambako alipigwa hadi kupoteza fahamu.

Aliyekuwa Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) Dk Namala Mkopi alisema Dk Ulimboka alipigiwa simu na watu ambao walimteka na kumpeleka porini nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam ambako alipigwa na kupoteza fahamu mpaka wasamaria wema walipomkuta asubuhi siku iliyofuata akiwa katika hali mbaya na kumpeleka kituo cha polisi.

Dk Ulimboka alitekwa saa sita usiku na watu watatu waliodaiwa kuwa na silaha aina ya short gun na bastola. Tukio hilo lilitokea eneo la barabara ya Tunisia, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam wa wakati huo, Suleiman Kova katika mkutano wake na waandishi wa habari alisema polisi wameanza uchunguzi wa kina juu ya kutafuta watu waliohusika katika tukio hilo na kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika.

Kamanda Kova alikanusha dhana kwamba tukio hilo limefanywa na wanausalama, huku akitaka raia wema kusaidia katika uchunguzi huo.

Kusisitiza katika hilo, Serikali iliahidi bungeni kuwa ingetoa  kauli juu ya hatua ambazo itazichukua dhidi ya madaktari, baada ya juhudi zote za kumaliza mgomo dhidi ya madaktari kushindikana.

Ahadi hiyo ya Serikali ilitolewa na Waziri Mkuu wa wakati huo, Mizengo Pinda mbele ya Bunge, kufuatia Naibu Spika wa Bunge wakati huo, Job Ndugai kuombwa muongozo na aliyekuwa Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi kuhusiana na mgomo huo wa madaktari.

Hata hivyo, mtu aliyetajwa kuwa ni raia wa Kenya, Joshua Mulundi alikamatwa baada ya kujitokeza na kutangaza kuhusika na tukio hilo na kufunguliwa kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi  Kisutu.

Agosti 6, 2012, aliyekuwa Mkurugenzi  wa Mashitaka (DPP), Dk Eliezer Feleshi  alimfutia kesi ya kujaribu kumuua na kumteka Dk Ulimboka baada ya kuona hana haja kuendelea kumshtaki kwa makosa hayo ambayo yalikuwa hayana dhamana na kisha siku hiyo akamfungulia kesi mpya ya kutoa taarifa za uongo polisi.

Hata hivyo, mahakama ilimkuta na hatia ya kutoa taarifa za uongo na ilimuhukumu kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya Sh1,000.

Mwandishi wa habari wa Redio Times, Chipangula  Nandule  aliyekuwapo mahakamani hapo alijitolea kumlipia faini hiyo ya Sh1,000 na sekunde chache baadaye askari polisi walimkamata Mulundi na askari hao kwa masharti ya kutotajwa majina yao gazetini kwa maelezo kuwa wao siyo wasemaji wa jeshi, walisema Mulundi ni raia wa Kenya, hivyo wanamshikilia ili waweze kuandaa taratibu za kumrejesha nchini kwao.

Kupotea kwa Saanane

Novemba mwaka jana kulitokea taarifa za kutoweka kwa  Ben Saanane baada ya chama chacke cha Chadema kutoa tamko rasmi kwamba hawajui alipo msaidizi huyo wa Mbowe.

Tangu kupotea kwa Saanane taarifa kutoka vyombo vya dola zimekuwa zikifanana kuwa ‘wanashughulikia’ kumtafuta.

Saanane alipotea katika mazingira ya kutatanisha na tangu kipindi hicho hadi sasa hajulikani alipo, huku familia yake na baadhi ya viongozi wa Chadema wakihofia kwamba huenda ameuawa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahi kunukuliwa akisema  hana uhakika kama mwanasiasa huyo chipukizi yupo hai ama ametangulia mbele ya haki. Hofu ya Waziri Mkuu na wengine inatokana na ukweli kwamba hakuna taarifa zozote za kiintelejinsia na polisi zinazoonyesha kama yupo hai, kwani hapatikani kwenye simu yake na hata kwenye makundi ya mitandao ya kijamii aliyojiunga.

Mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano, uenezi wa mambo ya nje wa Chadema, John Mrema amewahi kunukuliwa akisema, “…ni wakati wa polisi kutueleza wameshindwa nini kumpata Ben Saanane, mbona mtu akicomment kwenye magroup wanamtafuta na kumpata, kwani wameshindwa kumpata Ben au wanajua alipo?”.

Wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, Aprili mwaka huu, Freeman Mbowe alimuuliza Majaliwa kama vyombo vya ndani vya dola vimeshindwa kujua Saanane alipo kwa nini wasiombe ushirikiano kutoka nchi nyingine ikiwamo Uingereza kwa kitengo cha ‘Scotland Yard’ kama Kenya walivyofanya kumsaka kiongozi wa nchi hiyo Robert Ouko aliyefariki dunia, lakini baada ya kuchunguza wakapata taarifa.

Katika majibu yake, Majaliwa alisema uchunguzi wa suala la kutoweka kwa Saanane hauna kikomo na mara utakapokamilika Serikali itatoa taarifa yake.

Nape atishiwa bastola

Machi 23, 2017 aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alitishiwa bastola na mtu aliyeelezwa anatoka katika vyombo vya dola akiwa hajavaa sare yoyote, alipokuwa akijaribu kumzuia asizungumze na waandishi wa habari nje ya hoteli ya Protea, Dar es Salaam.

Nape alilazimika kuzungumza na waandishi akiwa amesimama juu ya gari nje ya ukumbi wa hoteli hiyo baada ya polisi kutaka kuuzuia mkutano huo usifanyike.

Hata hivyo, waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alisema kitendo cha askari  kuchomoa bastola hakikubaliki na alimwagiza mkuu wa jeshi la polisi kutumia picha zilizopigwa wakati wa tukio hilo kumsaka mhusika.

“Nape Moses Nnauye sio jambazi, ni Mtanzania, ni mbunge, mjumbe wa NEC wa CCM, hana rekodi ya uhalifu. Kitendo cha mtu kumtolea bastola sio cha kiaskari, sio cha Kitanzania na sio cha kiMungu, kama mtu ameweza kutoa bastola mbele ya kamera nawaza mbali ingekuwa kwenye uchochoroni angefanya nini,” aliandika Mwigulu kwenye ukurasa wake wa twitter.

“Nahusika na usalama wa raia wote wa Tanzania, nimemwelekeza IGP atumie picha kumsaka mtu yule aliyeinua kufanya kitu cha kihalifu kwa kofia ya uaskari. Na kama ni askari basi sheria zinazoongoza taasisi husika zichukue mkondo wake.”

Hata hivyo, hadi sasa hakuna majibu ya kujitosheleza kuhusu mtu aliyemchomolea bastola Nape.

Roma Mkatoliki atekwa

Aprili 2017, wasanii wa hip hop, Ibrahim Mussa maarufu kama Roma Mkatoliki, Monii Central Zone, Bin Laden na Imma ambaye ni mfanyakazi wa mama mzazi wa mmiliki wa studio za Tongwe Records iliyopo Masaki, Dar es Salaam, J Murder walitekwa na watu wasiojulikana  baada ya kuvamiwa.

Uvamizi huo ambao ulizua taharuki, ulidaiwa kufanyika saa 1:30 usiku. Kukamatwa kwa wasanii hao kulitafsiriwa kuwa ni mwendelezo wa tukio lililomkuta msanii Emanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego, ambaye alikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Morogoro na kisha kusafirishwa hadi Dar es Salaam kabla hajaachiwa kwa amri ya Rais John Magufuli.

Ingawa haikujulikana sababu za kutekwa Roma na wenzake, pia watekaji hawajafahamika mpaka sasa.

Tukio hilo lilimsukuma Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu (Chadema) kuomba mwongozo wa Spika katika mkutano wa Bunge uliopita.

Kutokana na ombi hilo, Spika wa Bunge, Job Ndugai aliiagiza Serikali kuchukua hatua haraka ili kufahamu ukweli wa suala hilo na kulipatia ufumbuzi.

Katika majibu yake, Ndugai alisema: “Katika hili niseme tu Serikali ilifuatilie haraka na kulipatia ufumbuzi maana siwezi kutoa ufafanuzi zaidi, maana ndio ninalisikia hapa kwako kwa mara ya kwanza.”

Hadi sasa bado hakuna majibu ya kina kuhusu tukio hilo.

Kibanda aumizwa vibaya

Machi, 2013 mwandishi wa habari ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda alinusurika kifo baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake kisha kupigwa na kujeruhiwa vibaya.

Kibanda alipigwa na kitu kizito chenye ncha kali kichwani, kutobolewa jicho la kushoto na kung’olewa ukucha wa kidole cha mkono na meno.

Katika tukio la Kibanda, inaelezwa kuwa watuhumiwa hao ambao hawajakamatwa walimtendea unyama huo akiwa anakaribia kuingia nyumbani kwake eneo la Mbezi Beach usiku wa saa sita akiwa ndani ya gari akingojea kufunguliwa geti.

Kibanda alisema kuwa akiwa amesimama langoni ghafla alishtukia gari lake likivunjwa kioo na katika harakati za kutaka kutambua nini kinaendelea, alivamiwa na watu hao.

Baada ya tukio hilo Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam liliwataka waandishi wa habari kushirikiana katika kutoa taarifa ya uchunguzi ya wahalifu waliomteka na kumjeruhi Kibanda.

Aliyekuwa kamanda wa kanda hiyo, Kova alisema kuwa ni mapema kuwabaini waliohusika katika tukio hilo. Kova alisema Kibanda ndiye anafaa kuwa shahidi wa kwanza katika tukio hilo wa kusema kilichotokea lakini kutokana na hali yake hawezi kuhojiwa hadi apate ahueni.

Kova alisema tukio hilo ni kubwa na Jeshi la Polisi Makao Makuu lilitoa askari wanne ambao wangeungana na wale wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ambao wamebobea katika uchunguzi. Hata hivyo, hadi sasa watuhumiwa wa tukio hilo la Kibanda bado hawajafahamika wala kukamatwa.

Ofisi za Immma zalipuliwa

Agosti mwaka huu ofisi za uwakili za Kampuni ya Immma Advocates zilizo chini ya wanasheria Fatuma Karume na wenzake zimechomwa moto na watu wasiojulikana na hadi sasa hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Profesa Safari azungumza

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari ameitaka Serikali kuchukulia mambo hayo kwa uzito wake yanapotokea, hususan yanayohusu usalama wa raia.