Matumizi holela ya dawa yachangia usugu katika matibabu

Mganga mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dk Charles Kiologwe.

Muktasari:

Kauli hiyo ilitolewa jana Jumamosi Agosti 12, 2018 na mganga mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dk Charles Kiologwe

Dodoma. Zaidi ya asilimia 60 ya dawa za antibayotiki zinatolewa na kutumika kimakosa mahali ambapo hazikupaswa kutumika.

Kauli hiyo ilitolewa jana Jumamosi Agosti 12, 2018 na mganga mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dk Charles Kiologwe wakati akifunga mafunzo ya matumizi sahihi ya dawa hizo kwa watoa huduma na wataalam wa afya mkoani hapa.

Mafunzo hayo yameandaliwa na mradi wa tuimarishe afya (HSPP) na kujumuisha wataalam na watoa huduma kutoka wilaya za mkoa huu.

Dk Kiologwe amesema kwa sasa Serikali haitalifumbia macho suala hilo kwa kuwa linasababisha upotevu wa rasilimali za nchi.

Amesema matumizi yasiyo sahihi yanaleta uharibifu rasilimali na madhara ya usugu katika matibabu kwa watumiaji.

“Kwa sasa bajeti ya dawa ni kubwa katika mkoa wa Dodoma kwa kipindi cha mwaka 2018/19 ni Sh4.3 milioni. Ni lazima tuhakikishe zinatumika vyema na si kuzifuja," amesema Kiologwe.

Meneja wa mradi wa HPSS Dodoma, Keneth Gondwe amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha watoa huduma kushiriki kikamilifu kuisaidia jamii na kupunguza usugu wa magonjwa.