Matumizi ya dawa yanavyoweza kuhatarisha figo

Mkuu wa Kitengo cha Figo Katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Jaqueline Shoo (kushoto) akionyesha namna mashine ya figo bandia ‘dialysis’ inavyofanya kazi ya kumsaidia mgonjwa kuondoa sumu na maji yasiyohitajika mwilini. Picha na Herieth Makwetta

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, matumizi ya dawa za kupunguza maumivu jamii ya diclofenac na umezaji wa dawa pasipo kupata ushauri wa daktari, ni sababu nyingine ya kuharibu figo.

 Watu wanaotumia dawa katika maisha yao yote wakiwamo wanaougua kisukari, moyo na shinikizo la damu, wapo hatarini kupata maradhi ya figo.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, matumizi ya dawa za kupunguza maumivu jamii ya diclofenac na umezaji wa dawa pasipo kupata ushauri wa daktari, ni sababu nyingine ya kuharibu figo.

Pengine hii ni sababu ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kupokea zaidi ya wagonjwa 1,300 wanaotibiwa katika kliniki za figo, huku 176 wakisafishwa damu kila mwezi huku ikielezwa kuwa Serikali imeshapeleka zaidi ya wagonjwa 160 kubadilishwa figo nje ya nchi kwa mwaka 2013/16.

Mkuu wa Kitengo cha Figo na daktari bingwa wa maradhi ya figo Muhimbili, Jacqueline Shoo alisema asilimia kubwa ya wagonjwa wamekuwa wakiugua kisukari, shinikizo la damu, matatizo ya moyo na maradhi mengine yanayowafanya wanywe dawa katika maisha yao yote.

Alisema wapo wanaopata tatizo la kuziba kwa njia ya mkojo inayosababishwa na saratani ya tezi dume, magonjwa ya njia ya mkojo yanayosababisha saratani, matumizi ya mitishamba na dawa ambazo zinatumika bila viwango.

“Matumizi ya muda mrefu ya dawa za maumivu jamii ya diclofenac ni moja ya sababu ya figo kupoteza nguvu ya kufanya kazi,” alisema Dk Shoo.

Alisema mgonjwa anapofika kitengo hicho, huangaliwa kiwango cha sumu katika damu, magonjwa yanayoambatana nayo, upungufu wa madini au yaliyozidi na hutoa tiba inayotakiwa kulingana na tatizo husika.

Dk Shoo alisema pia huangalia viwango vya maji kama yamezidi, ushauri wa chakula kipi kinawafaa ili kuhakikisha afya zao zinarudi katika hali nzuri kabla ya kuanza kutoa matibabu.

Akizungumzia matibabu kwa watu ambao wamefikia daraja la tano la ugonjwa huo, Dk Shoo alisema wanapaswa ama kupandikizwa figo au kupata huduma ya kusafishwa damu kwa maisha yao yote.

Gharama

Dk Shoo alisema matibabu ya figo ni ya gharama na wananchi wengi hawamudu.

Alisema gharama ya huduma ya kusafishwa damu ni Sh300,000 na mgonjwa anatakiwa kwa wiki kufanyiwa kati ya mara tatu hadi nne, hivyo gharama kuwa kati ya Sh900,000 na Sh1.2 milioni.

Mkuu wa kitengo cha kusafisha damu kupitia figo bandia, Judith Mwaipopo alisema Muhimbili ilianza kutoa huduma hiyo Mei mwaka 2011 wakihudumia wagonjwa watano kwa mashine saba walizokuwa nazo.

Alisema mwaka 2014, mashine ziliongezwa na kufikia 10, hivyo kutoa huduma kwa wagonjwa 30 kwa wiki.

Alisema baada ya kupanua kitengo hicho Agosti, sasa kinahudumia wagonjwa 174 kwa kutumia mashine 43, huku kila wiki wakiongezeka wagonjwa sita wa kusafisha damu na wakati mwingine kufikia 17 kwa mwezi.

Hata hivyo, alisema kuna changamoto ya rasilimali watu kwani licha ya wagonjwa kuongezeka, idadi ya wafanyakazi ni ileile.

Alisema kitengo hicho kina wafanyakazi 19 na kwamba, kila mmoja anahudumia wagonjwa saba badala ya watatu anaopaswa kuwahudumia.