Maua Sama, Soudy Brown waendelea kusota rumande

Muktasari:

Walikamatwa na polisi baada ya kuweka video mtandaoni inayowaonyesha mashabiki wakikanyaga fedha wakati  wakicheza wimbo ‘Iokote’ wa Maua Sama

 Dar es Salaam. Mwanamuziki anayetamba na wimbo ‘Iokote’ Maua Sama na mtangazaji wa kipindi cha Shilawadu, Soudy Brown wameendelea kusota rumande tangu walipokamatwa Septemba 16, 2018.

Wasanii hao walikamatwa sambamba na meneja wa Maua, Fadhili Kondo na wote wanashikiliwa kwa kosa la uharibifu wa mali ya umma baada ya kuonekana mtandaoni wakirusha hela na kuzikanyaga.

Akizungumza na MCL Digital leo Jumatano Septemba 19, 2018 msemaji wa nyumba ya vipaji (THT),  Rehema Jones amesema mpaka sasa watatu hao bado wanashikiliwa na polisi.

Akielezea zaidi Rehema amesema walikamatwa Jumapili na taarifa za kukamatwa kwao zilifika THT siku ya Jumatatu.

Alipoulizwa kuhusu maendeleo yao na iwapo wanatarajiwa kufikishwa mahakamani Rehema amesema, “utaratibu ndio unafanyika kuhusu suala la Mahakama na sisi tunasubiri kuona nini kitaendelea, kwa sasa hatuna zaidi cha kuzungumza.”

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu idadi ya wasanii ambao inasemekana wameendelea kukamatwa kufuatia sakata hilo, Rehema amesema; “THT ina taarifa za watu watatu tu, hao wengine hatuwezi kuwazungumzia.

Mwandishi wa MCL Digital ambaye yupo katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam, anaripoti kuwa kitengo kinachoshughulika na makosa ya mtandao kimemweleza kuwa hakiwezi kutoa taarifa kwa kuwa wao si wasemaji.

“Nimeelezwa kuwa taarifa kuhusu watuhumiwa hao nitaipata kwa Kamanda wa Kanda kwa kuwa wao kazi yao ni kuwahoji watuhumiwa na kutafuta ushahidi kisha wanakabidhi kwake,” anasema Fortune.

Alipomtafuta Kamanda wa Kanda Maalum, Lazaro Mambosasa alimweleza kuwa yupo katika ziara ya kikazi Kigamboni jijini Dar es Salaam na kumuomba amtafute jioni ampatie taarifa kamili.