Maumivu ya nyonga yaendelea kumtesa mtu mrefu

Baraka Elias

Muktasari:

Elias alianguka nyumbani kwake mkoani Ruvuma na alikuja Dar es Salaam kwa ajili ya kufuatilia matibabu ambayo mpaka sasa yamekuwa magumu kupatikana ikielezwa kwamba umbo lake pia linachangia.

Dar es Salaam. Mtu mrefu zaidi, Baraka Elias bado  amesema umepita mwezi mmoja na nusu sasa hajaambiwa chochote kuhusu matibabu ya nyonga inayomsumbua baada ya kuanguka.

Elias alianguka nyumbani kwake mkoani Ruvuma na alikuja Dar es Salaam kwa ajili ya kufuatilia matibabu ambayo mpaka sasa yamekuwa magumu kupatikana ikielezwa kwamba umbo lake pia linachangia.

Mtu huyo mwenye urefu wa futi 7.4 amemwambia mwandishi wa habari hizi kuwa hafahamu chochote kinachoendelea kuhusu matibabu yake zaidi ya kuzidi kupata maumivu.

Anasema mara ya mwisho alikwenda Taasisi ya Tiba ya Mifupa (Moi) ambako alitakiwa kufanyiwa upasuaji na kuambiwa kuwa angepewa taarifa.

“Hakuna dawa wala kliniki ninayohudhuria, hali yangu inazidi kuwa mbaya naomba msaada jamani nitibiwe napata maumivu,” amesema.

Elias alipata matatizo ya nyonga Aprili 2016 baada ya kuanguka nyumbani kwake Mbinga mkoani humo na kutibiwa Hospitali ya Peramiho na baada ya kushindikana alipewa rufaa ya kwenda Moi alikotakiwa kufanyiwa upasuaji, lakini ilishindikana kutokana na mifupa yake kuwa mirefu kupita kiasi hivyo kukosekana nyonga ya saizi yake.

Mkurugenzi wa Moi, Dk Othman Kiloloma amesema: “Vipimo vyote vimeshafanyika na tumetuma kwa wataalamu wanatengeneza vifaatiba kulingana na mifupa yake, tumeagiza vya aina tatu.”