Mauzo katika soko la Hisa Dar es Salaam yaporomoka

Muktasari:

Ripoti ya wiki ya soko hilo inabainisha kushuka mauzo kwa asilimia 91, huku idadi ya hisa zilizouzwa zikishuka kwa asilimia 94.

Dar es Salaam. Hali siyo nzuri katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) baada ya mauzo kuporomoka kwa kishindo huku idadi ya hisa ikishuka.

Ripoti ya wiki ya soko hilo inabainisha kushuka mauzo kwa asilimia 91, huku idadi ya hisa zilizouzwa zikishuka kwa asilimia 94.

Mauzo hayo yamepungua kutoka Sh32.5 bilioni wiki iliyopita mpaka Sh3 bilioni kwa juma lililoishia Oktoba 13, baada ya hisa zilizouzwa kushuka kutoka milioni tisa mpaka 500,000.

Meneja Miradi na Biashara wa DSE, Patrick Mususa alisema hali hiyo ni ya kawaida na inadhihirisha uhuru wa soko kwa wawekezaji wa ndani na nje na kwamba, hakuna kampuni au mtu anayeweza kupanga mwenendo wake.