Mavunde aitaka jamii kusaida wenye ulemavu

Muktasari:

Amesema watu wenye ulemavu wana mahitaji mengi ambayo ni vyema watu wa kada mbalimbali kujitolea kuwasaidia

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu, Antony Mavunde, ameitaka jamii kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuisaidia jamii ya watu wenye ulemavu kwa kuwapa elimu itakayowasaidia kujiepusha na madhara kama ajali za barabarani.

Mavunde aliyasema hayo leo Jumapili Septemba 9, 2018 jijini i Dar es Salaam wakati akifunga mafunzo ya utambuzi wa alama za barabarani na uchoraji, kwa wanafunzi kutoka shule za msingi za mkoa huo yaliyokuwa yakitolewa na Kampuni ya Amend, chini ya ufadhili wa kampuni ya mafuta ya Puma Tanzania.

Amesema tangu kampeni ya usalama barabarani ianze 2013, imekuwa ikilenga kupunguza ajali za barabani na mafanikio yameanza kuonekana.

“Tangu ilipozinduliwa kampeni hii tunaona kuna mafanikio na katika awamu ya kwanza ya mafunzo haya, wanafunzi 9,152, wamepewa mafunzo ya usalama barabarani kwa kushiriki pia katika michoro, hongereni sana Puma,” amesema.

“Kinachofurahisha zaidi ni hatua ya kuzishirikisha shule za wanafunzi wenye ulemavu.”

Amesema watu wenye mahitaji ni kundi lenye changamoto nyingi ambazo kimsingi kama jamii itaamua kushirikiana kwa pamoja kuzitatua kama ilivyofanya Puma Tanzania, nchi itakuwa imetimiza ndoto zao za baadaye.

Amesema suala la kupungua kwa ajali za barabarani kwa kundi la wanafunzi kwa shule ambazo zimepewa mafunzo hayo tangu mpango huo kuanza ni jambo la kupongezwa kwa kuwa limesaidia kuleta mabadiliko chanya kwa jamii.

Awali, Meneja Mkuu wa Puma Tanzania, Philippe Corsaletti, amesema mafunzo hayo ni mwendelezo wa kuwaelimisha wanafunzi kuhusu usalama barabarani.

Amesema tangu kuanza kwa kampeni hiyo, tayari wamewafikia wanafunzi 68,000 katika shule 63 za mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Geita, Kilimanjaro na Ruvuma.

Kwa mwaka huu pekee, kampuni hiyo imetoa mafunzo kwa wanafunzi 9,152 kutoka shule 16 za mikoa ya Dar es Salaam na Ruvuma.

Mratibu wa Usalama Barabarani kutoka Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mbunja Matibu, mbali na pongezi alizozitoa, alisema suala la elimu ya usalama barabarani ni jambo mtambuka linalopaswa kuungwa mkono na jamii.

Mpango huo pamoja na mambo mengine umelenga kuwapa elimu wanafunzi itakayowasaidia kujiepusha na ajali za barabarani.

Mwaka huu mafunzo hayo yamezihusisha shule za Rutihinda ya mkoa wa Dar es Salaam na Mnyonga ya mkoani Ruvuma.

Katika mashindano hayo, mshindi wa kwanza aliibuka mwanafunzi Francisco Salvatory wa Shule ya Msingi Upanga aliyejinyakulia Sh500,000 wa pili ni Magreth Andrew wa Shule ya Msingi Maktaba, aliyezawadiwa Sh300,000 na nafasi ya tatu imechukuliwa na mwanafunzi wa shule ya Msingi Upanga aliyezawadiwa Sh150,000