Mavunde asema vijana 30,000 kunufaika na mafunzo ya kilimo na ujasiriamali

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde 

Muktasari:

Amesema kiasi cha Sh11bilioni kitatumika kama mtaji na kuanzisha shughuli za uzalishaji

Iringa.  Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde amesema vijana 30,000 wa mikoa ya Iringa, Mbeya na visiwani Zanzibar watanufaika na fursa ya mafunzo ya kilimo na ujasiriamali katika Program ya Feed the Future.

Amesema programu hiyo inayofadhiliwa na Shirila la Kimataifa la Misaada la Marekani (USAID), vijana watapewa nyenzo na mitaji ya kuanzia shughuli za uzalishaji mali yenye thamani ya Sh11bilioni.

Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Agosti 21, 2018 mkoani Iringa wakati akizindua baraza la vijana la ushauri wa mradi, kulitaka baraza hilo kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa hasa katika kumkomboa kijana wa Kitanzania na changamoto za ukosefu wa ajira na kumsaidia kufikia malengo yake.

Kwa upande wake kaimu mkuu wa Mkoa wa Iringa, Richard Kasesela ameahidi kutoa ushirikiano wakati wote wa utekelezaji wa mradi huo ambao utawanufaisha vijana wa Iringa kwa kiasi kikubwa.

Awali,  akimkaribisha Mavunde, Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Dk  Inmi Patterson amesema nchi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza ujuzi wa nguvu kazi ya vijana nchini kwa kuhamasisha ushiriki wao katika sekta ya kilimo ili kuongeza pato la Taifa zaidi kupitia sekta ya Kilimo.