Mavunde awataka wananchi kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa

Muktasari:

Naibu Waziri Anthony Mavunde amezindua mfumo wa Taifa wa Huduma za Hali ya hewa leo.


Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde amewataka wananchi kujenga utaratibu wa kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa ili kujikinga na kujiandaa na maafa yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi.

Ametoa rai hiyo leo Jumanne Agosti 21, 2018 katika uzinduzi wa Mfumo wa Taifa wa Huduma za Hali ya Hewa (NFCS) jijini hapa.

Amesema ili nchi iweze kupata maendeleo, utekelezaji wa udhibiti wa majanga yatokanayo na hali ya hewa ni muhimu kuzingatiwa.

“Mfano asilimia 60  ya wananchi wamejikita katika kilimo na uvuvi lakini hawawezi kufanikiwa kama kazi zao zitaathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa," amesema Mavunde na kuwataka wananchi kutofuata utabiri wa hali ya hewa wa mitaani.

“Watu wanapuuza  utabiri wa hali ya hewa na kujikuta wakipata madhara makubwa ikiwemo mafuriko na kusababisha wengine kukosa makazi ya kuishi.”

Amebainisha kuwa magonjwa ya mimea, wakulima kukosa mavuno na kuongezeka kwa kina cha bahari ni moja ya athari zitokanazo na  mabadiliko  ya hali ya hewa, kubainisha kuwa  ni muhimu kuzingatia utabiri sahihi na wa kitaalam.

Amesema mfumo huo wa NFCS utasaidia kuboresha utoaji wa taarifa na matumizi ya huduma za hali ya hewa na kufanya maamuzi mapema.

"Pia lengo ni kuwajengea uwezo wananchi kuhusu athari zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa kwa sababu wengi wamekuwa wagumu kufuatilia taarifa mbalimbali,” amesema.

Kwa upande wake mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), Agnes Kijazi amesema licha ya wananchi kuwa na uelewa wa kufuatilia taarifa za hali ya hewa bado uzingatiaji unahitajika ili kukabiliana zaidi na athari zinazotokea.

Amebainisha kuwa mfumo huo utasaidia kuboresha matumizi sahihi ya hali ya hewa na kupunguza majanga ikiwemo mafuriko ambayo hutokea mara kwa mara.

"Tanzania kama nchi nyingine mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo ukame, mafuriko na maradhi vinaweza kuepukika endapo tutaendelea kuwajengea uwezo watoaji na watumiaji wa huduma za hali ya hewa," amesema.