Mawakili 24 Uganda wajitosa kumtetea Bobi Wine

Muktasari:

Kaggwa amewahakikishia wanasheria hao kwamba atafuata katiba inavyosema ili kuhakikisha haki inatendeka kumuokoa Bobi Wine.

Kampala, Uganda. Timu ya mawakili maarufu 24 wameungana kumtetea Mbunge wa Kyadondo, Robert Kyagulanyi  maarufu kama Bobi Wine, huku wakimtaka Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu nchini Uganda, Med Kaggwa kuhakikisha anatumia vyema haki ya kikatiba ili kuhakikisha haki inatendeka.

“Kipindi hiki tunaamini kwamba Tume ya Haki za Binadamu ya Uganda itakuja na kauli kuhusiana na sakata hili. Tunatambua kuwa (Kaggwa) unayo mamlaka hayo,” amesema Erias Lukwago, mmoja wa wanasheria wa utetezi.

Kifungu cha sheria cha 53(2) cha katiba kinasema kwamba Tume inaweza kujiridhisha kwamba kuna uingiliaji wa haki za binadamu na uhuru (a) mtu aliyewekwa kizuizini (b) kuwapo kwa malipo ya fidia.

Katika mkutano wa Tume uliofanyika makao makuu mtaa wa Lumumba jijini Kampala, wanasheria hao wameibua hoja ya kuzuiwa kupatiwa matibabu, kupata usaidizi wa kisheria, kuzuiwa kuonana na familia pamoja na kuzungumza na waandishi wa habari kama makosa ya kuminya haki za utu.

Pia wamezungumzia kuhusu polisi pamoja na maagizo kutoka mamlaka za juu kuzuia matumizi ya simu kwa watuhumiwa kuwasiliana na watu wengine.

Hata hivyo, Kaggwa amewahakikishia wanasheria hao kwamba atafuata katiba inavyosema ili kuhakikisha haki inatendeka kumuokoa Bobi Wine.

“Tunatakiwa kuwa mstari wa mbele kupigania haki, siwaamini kabisa polisi kwamba wanaweza kumpatia mwanasheria Bobi Wine, kinachotakiwa ni sisi wenyewe kuhakikisha tunasimamia hili,” amesema Kaggwa.

Kwa mujibu wa  ripoti mbalimbali za vyombo vya habari, mbunge huyo ambaye pia ni mwanamuziki ana matatizo ya figo ambayo yanahitaji kutibiwa ipasavyo na madaktari bingwa waliobobea.