Mawakili wa Lema wapinga vielelezo vya jamhuri

Muktasari:

Wamepinga vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani leo Jumanne na upande wa jamhuri kwa madai kwamba  vimeokotwa mtaani

Arusha. Mawakili Sheck Mfinanga na John Mallya ambao wanamwakilisha mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema katika kesi ya kudaiwa kumdhalilisha Rais John Magufuli wamepinga vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani leo Jumanne na upande wa jamhuri kwa madai kwamba  vimeokotwa mtaani.

Mawakili hao wamepinga vielelezo hivyo ambavyo ni kanda za video zinazomwonyesha Lema akiwa katika eneo la mkutano Oktoba 22 mwaka juzi katika eneo la Kambi ya Fisi jijini Arusha akitamka maneno yanayodaiwa kumdhalilisha Rais Magufuli.

Vielelezo hivyo vilivyowasilishwa leo Jumanne na shahidi wa  sita upande wa jamhuri, Inspekta Aristides (44) ambaye ni ofisa wa polisi idara ya uchunguzi na kisayansi makao makuu ya upelelezi jijini Dar es Salaam.

Shahidi huyo ambaye ni mchunguzi wa picha za video na sauti alifika mbele ya mahakama hiyo  na kuwasilisha vielelezo vyake  na kusema kwamba Novemba 21 mwaka juzi akiwa ofisini kwake alipokea kanda za video aina ya Sonny  kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha vikiwa vimefungwa kwenye bahasha.

Shahidi huyo aliiambia Mahakama kwamba baada ya kupokea alianza kufanyia uchunguzi ili kubaini ni halisi au la na baada ya kuchunguza aliandika taarifa ya uchunguzi na kisha kuitoa video hiyo kutoka kwenye tape kwenda kwenye CD.

Akijibu swali lililoulizwa na wakili wa upande wa jamhuri Agnes Hyera kwamba ana maoni gani kuhusu vielelezo hivyo shahidi huyo aliiomba mahakama hiyo ipokee vielelezo hivyo kama ushahidi katika kesi hiyo.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Arumeru, Devotha Msofe wakili wa upande wa utetezi Mallya alipinga uwasilishwaji wa vielelezo hivyo kwamba una mapungufu ya kisheria kwa kuwa shahidi huyo sio yeye aliyerekodi kanda hizo na hivyo hakustahili kuuwasilisha mbele ya mahakama hiyo.

Akiunga mkono hoja ya Mallya wakili upande wa utetezi Mfinanga aliiambia mahakama hiyo kwamba shahidi huyo alitumiwa kanda hizo akiwa jijini Dar es Salaam na kimsingi hastahili kusimulia kitu ambacho hajakiona.

Mara baada ya hoja hizo ndipo mawakili wa upande wa jamhuri waliomba  hairisho fupi kwa muda wa nusu saa ili wakazipitie hoja za upande wa utetezi na ndipo Hakimu Msofe aliridhia na kisha kuhairisha kesi hiyo kwa muda huo.

 

Mara baada ya kurejea mahakamani wakili upande wa jamhuri, Hyera alijibu hoja hizo na kusema kwamba wanapinga  hoja zilizotolewa na mawakili upande wa utetezi kwa kuwa shahidi huyo ndiye aliyezifanyia uchunguzi kanda hizo za video na kisha kuzifunga kwa  kuweka lakili  na kutia muhuri kabla ya kuvirudisha Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha.

Hata hivyo, mawakili wa upande wa utetezi walipinga tena hoja hiyo na kuiambia Mahakama kwamba hawawezi kukubali kitu kilichookotwa mtaani lazima wajiridhishe na kanda hizo na kwamba shahidi huyo alipaswa kuwa na mahusiano ya karibu na kanda hizo.

Mara baada ya hoja hizo ndipo Hakimu Msofe alihairisha kesi hiyo hadi Febuari 16 mwaka huu ambapo anatarajia kutoa uamuzi kuhusu endapo vielelezo hivyo vinastahili kupokelewa mahakamani kama ushahidi au la.