Mawakili wachuana kuhusu dosari za mashahidi wanane

Washtakiwa katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Erasto Msuya, wakiingia katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi jana. Picha na Daniel Mjema

Muktasari:

  • Akiwasilisha hoja kwa niaba ya wenzake, wakili Majura Magafu alienda mbali na kudai dosari zilizopo katika maelezo hayo ni kubwa, haziipi mahakama utashi wa kuamua kuzipokea.

Moshi. Mawakili wa utetezi kesi ya mauaji ya Erasto Msuya, jana waliwasilisha dosari za kisheria katika maelezo ya mashahidi wanane ambao hawapatikani, wakidai hazistahili kupokelewa kama kielelezo.

Akiwasilisha hoja kwa niaba ya wenzake, wakili Majura Magafu alienda mbali na kudai dosari zilizopo katika maelezo hayo ni kubwa, haziipi mahakama utashi wa kuamua kuzipokea.

Magafu anayesaidiana na Hudson Ndusyepo, Emmanuel Safari na John Lundu, aliwasilisha hoja hizo mbele ya Jaji Salma Maghimbi wa Mahakama Kuu anayesikiliza kesi hiyo.

Aliieleza mahakama kuwa kifungu cha 10 (3) cha Sheria ya Uendeshaji Mashauri ya Jinai (CPA) sura ya 20 ya mwaka 2002, lazima shahidi aliyetoa maelezo na polisi aliyeandika wasaini katika maelezo hayo.

“Akishamaliza (polisi) kuandika maelezo lazima ampe shahidi ayasome na kuyasaini chini ya mstari wa mwisho wa maelezo yake na kuandika uthibitisho kuwa, ameyaandika kwa uaminifu,” alieleza.

Hata hivyo, Magafu alidai maelezo ya shahidi Ramadhan Abdallah yanayotakiwa kupokelewa aliyoyaandika Agosti 12, 2013 saa 6:00 mchana ofisi ya RCO Arusha, hakuyasaini na badala yake iliwekwa alama X.

“Katika hii statement (maelezo) ukiangalia huku pembeni inaonekana kama amesaini, lakini hii siyo saini inayotakiwa kwa mujibu wa kifungu hicho cha 10(3) cha CPA,” alidai wakili huyo.

Akichambua maelezo ya Hamisa Kassim maarufu Ndege Ulaya aliyesajili laini za simu zinazodaiwa kutumika kumvuta marehemu eneo la tukio, Magafu alidai hata hiyo haikusainiwa.

Magafu alidai maelezo hayo yaliyoandikwa Agosti 10, 2013 katika ofisi ya RCO bila kutaja ni mkoa gani, yanaonyesha shahidi huyo alisaini pembeni ukurasa wa 2,3,4 badala ya eneo sahihi.

“Aliyerekodi haya maelezo hakuyasaini kwenye uthibitisho na vilevile signature (saini) inayodaiwa ni ya shahidi haikusainiwa kwa mujibu wa sheria inavyotaka isainiwe chini ya mstari wa mwisho,” alidai.

Maelezo mengine ni ya Adam Leani maarufu Mongululu anayedaiwa kutumwa kwenda kusajili laini zilizotumika katika mipango ya mauaji hayo, iliyoandikwa ofisi ya RCO Arusha Agosti 12, 2013.

“Hii statement (maelezo) ina matatizo mawili. Uthibitisho wa mwandishi haikusainiwa na vilevile shahidi mwenyewe amesaini tu baada ya maelezo, alitakiwa asaini chini ya mstari,” alieleza.

Wakili huyo alidai maelezo ya mashahidi watano waliobaki, waliweka saini baada ya sentensi ya mwisho ya maelezo badala ya chini ya mstari kama sheria hiyo ya CPA inavyotaka.

Maelezo hayo ni ya mashahidi Shaaban Mahamoud aliyoyaandika Septemba 15, 2013; na ya Evelyne William yaliyoandikwa Agosti 14, 2013 yote yaliandikwa na mkaguzi msaidizi Damian Chilumba.

Aliendelea kuwa maelezo mengine ni ya Mohamed Juma yaliyoandikwa ofisi ya RCO Arusha Agosti 12, 2013 ofisi ya RCO Arusha na konstebo Seleman Faraji wa kitengo cha makosa ya kimtandao.

Maelezo mengine ni ya Godson Mangeki yaliyoandikwa Agosti 14, 2013 na konstebo Seleman na ya Pius Shija yaliyoandikwa Agosti 10, 2013 katika ofisi ya RCO Arusha na sajenti Herman Ngurukizi.

Hoja nyingine iliyowasilishwa na Magafu kwa niaba ya wenzake, ni madai ya kukiukwa kwa kifungu cha 34B (2) (c) cha sheria ya ushahidi kama ilivyofanyiwa marejeo na Bunge mwaka 2002.

“Kifungu hicho kinasema lazima maelezo ya shahidi yawe na uthibitisho wake mwanzoni kabisa kabla hajaanza kuandika maelezo yake mbele ya polisi, kwamba atatoa maelezo ya kweli tu,” alidai Magafu na kuongeza: “Anatoa uthibitisho (shahidi) kuwa maelezo atakayoyatoa yatakuwa ya kweli bila hila na kama yatathibitika ni ya uongo, atashitakiwa mahakamani kwa kutoa maelezo ya uongo.

“Kilichopo kwenye haya maelezo yote shahidi anasema ‘maelezo niliyoyatoa ni kweli kwa ufahamu wangu’, badala ya kusema ‘maelezo nitakayoyatoa yatakuwa ya kweli kadiri ya ufahamu wangu.

“Concern (hoja) yetu kubwa ni haya maneno ambayo yanaonyesha tayari alitoa uthibitisho wakati statement yenyewe alikuwa hajaandika. Hii ni kasoro kubwa ya kisheria.

“Masharti ya Police Form 2A (inayotumika kuchukua maelezo) masharti yake yalinukuliwa kwa wakati uliopita akisema maelezo niliyoyatoa, badala ya maelezo nitakayotoa.”

Magafu alidai utata wa aina hiyo uliwahi kuamuliwa na majaji wa mahakama ya rufani katika kesi namba 40/2014, ya Elias Kivuyo dhidi ya Jamhuri jijini Arusha ambao waliweka msimamo wa sheria.

“Majaji walisema ili maelezo ya shahidi ambaye hapatikani yaweze kupokelewa, lazima mahakama ijiridhishe kuwa matakwa ya kifungu cha 34B (2) (a-f) cha sheria ya ushahidi yamefuatwa kikamilifu,” alieleza Magafu na kuongeza:

“Kufuatwa kwa kifungu hicho ni pamoja na kujiridhisha kuwa maelezo hayo yamesainiwa na shahidi lakini maelezo yote haya hayajakidhi takwa hili. Pia, uthibitisho wake ulitolewa kimakosa.

“Kasoro tulizozieleza ni kubwa na haziipi mahakama utashi wa kuzipokea haya maelezo. Hizi statements siyo statements kwa maana ya sheria hivyo hazitakiwi kupokelewa kwa namna yoyote.”

Baada ya kuwasilisha hoja hizo, wakili wa Serikali mwandamizi, Abdallah Chavula anayesaidiana na Kassim Nassir, alieleza kuwa hawakubaliani na mapingamizi zilizowasilisha na upande wa utetezi.

Chavulla alikiri kwamba kifungu cha 10 (3) cha CPA, mashahidi Hamisa Kassim na Ramadhan Abdallah, walitakiwa kusaini maelezo yao chini ya mstari wa mwisho wa maelezo yake polisi.

“Wenzetu wanakiri kwamba katika maelezo mengine yote sita yaliyosalia, sahihi inaonekana imewekwa pembeni ya mstari wa mwisho. Ukiangalia maelezo ya Hamisa pembeni ya mstari iko sahihi yake,” alisema Chavula na kuongeza:

“Ni maoni yetu kuwa si sahihi kusema hakuna saini kwenye maelezo hayo. Ukichunguza kwa umakini utagundua maelezo yote yamesainiwa ila yamesainiwa pembeni mwa sentesi ya mwisho.”

Hata hivyo, Chavulla alidai kuwa upande wa mashtaka unakubaliana na hoja za mawakili wa utetezi kuwa maelezo ya shahidi Abdallah hakuyasaini baada ya kuyaandika polisi.

Chavula alieleza kuwa ni kweli matakwa ya sheria yanataka saini kuwekwa chini ya mstari, lakini kitendo cha shahidi kusaini sehemu isiyoelekezwa na sheria, haisababishi maelezo kuwa mabovu.

Kuhusu uthibitisho kutumia sentensi ya wakati uliopita badala ya wakati uliopo, alidai mazingira ya kesi iliyonukuliwa na mawakili wa utetezi ni tofauti na mazingira ya kesi iliyopo mbele yao.

“Ukiangalia hii statement ya Mahmoud ameanza kwa kusema this statement i make (maelezo haya ninayoyatoa) siyo past tense (wakati uliopita) kama wenzetu walivyojenga hoja yao,” alidai.

Chavula alidai maneno I make this statement, yanaonekana pia katika maelezo ya mashahidi aliowataja kuwa ni Hamisa, Adam, Mohamed, Evelyne, Godson.Aneth na Ramadhan.

“Kwa kuwa kwenye kesi waliyoinukuu wenzetu wanasema maelezo tuliyowapatia yana dosari. Kwenye maelezo yetu kunaonekana maneno I make this statement na siyo I made this statement,” alidai Chavula.

Akijibu hoja ya polisi walioandika maelezo hayo kutoweka sahihi zao, Chavulla alieleza kuwa hakuna sheria inasema lazima aweke saini yake na kwamba siyo dosari kutoweka saini.

Kutokana na hoja hizo, Chavulla aliiomba mahakama kuyatupa mapingamizi hayo na kupokea maelezo hayo kama ushahidi kwa vile matakwa yote ya kisheria yalizingatiwa hatua zote.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Maghimbi aliahirisha kesi hiyo hadi leo saa 4:30 asubuhi wakati atakapotoa uamuzi mdogo iwapo maelezo hayo yapokelewe au la.

Msuya aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa ndani na nje ya Arusha, aliuawa kwa kutumia bunduki ya kivita ya Sub Machine Gun (SMG) Agosti 7, 2013 eneo la Mijohoroni Hai, mkoani Kilimanjaro.