Mawaziri, naibu mawaziri wapangua hoja za wabunge

Muktasari:

  • Mawaziri na manaibu mawazi wameungana kupangua  hoja za Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka wa fedha 2019/20 zilizotolewa na wabunge kwa wiki nzima.

Dodoma. Mawaziri na manaibu waziri zaidi ya sita na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Adelaedus Kilangi wameunganisha nguvu kupangua hoja za wabunge katika Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka wa fedha 2019/2020.

Wakichangia mpango huo bungeni leo Jumatatu Novemba 12, 2018, mawaziri hao wamejibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge walizozitoa wakati wakiuchangia mpango huo.

Naibu Waziri wa Maji, Juma Aweso amesema tatizo la maji nchini  litakuwa historia baada ya Serikali kupata fedha kutoka Serikali ya India Dola za Marekani 500milioni .

Amesema mradi huo utatekelezwa katika miji 26 na kwamba, atakaa na wabunge wanaotoka katika miji hiyo kuwaelezea juu ya miradi hiyo.

Pia, amesema kuna fedha Dola za Marekani 350 milioni kutoka Benki ya Dunia ambazo zitatumika kuhakikisha kuwa miradi ya maji vijijini inakuwa endelevu.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kitaifa na Kikanda, Dk Damas  Ndumbaro amesema Tanzania ina mahusiano mazuri ya kiuchumi, kisiasa, kijamii, kiusalama na kidoplamasia, hali inayotokana na balozi zilizoko nje ya nchi kufanya kazi vizuri.

“Mabalozi wetu wanafanya kazi nzuri ya kuvutia wawekezaji na utalii ndiyo maana kuna ongezeko la watalii wanaokuja hapa nchini. Tunahakikisha tunakuwa chachu ya utekelezaji wa mambo mbalimbali maana mikopo nafuu,” amesema.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema wamevirejesha serikalini viwanda  vya kuchakata nyama katika mikoa ya Shinyanga na Mbeya.

Amesema pia wameanzisha dawati la sekta binafsi la kutatua changamoto za sekta binafsi na kuwapatia mitaji.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema hoja walizotoa wabunge zitazingatiwa wakati wa bajeti ya 2019/20.

Kuhusu ubora wa elimu kuwa idadi ya wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na sekondari hailingani na miundombinu, Profesa Ndalichako amesema maofisa elimu hivi sasa wanaendelea uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza ni  lazima wazingatie suala hilo.

Kwa upande wa wanafunzi wanaohamishwa vyuo baada ya vyuo kufungwa kubadilishiwa kozi, amesema chuo kinapofungiwa wanalazimika kuwahamisha wanafunzi kulingana na kozi zao walizokuwa wanasomea na si vinginevyo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema mpango huo umefungamanisha ukuaji wa uchumi na afya za Watanzania.

Amesema katika mwaka wa fedha  2017/18 watumishi 8000 katika sekta ya afya wameajiriwa.

“Bajeti ya dawa imeongezeka kufikia  Sh270 bilioni kutoka Sh30 bilioni na Sh9 bilioni zitatumika katika vifaa tiba,” amesema.

Waziri wa Madini, Angelah Kairuki amesema ukuta wa Mererani umeongeza mapato yatokanayo na madini katika eneo hilo kwa asilimia 10.

Amesema wamefanya ukaguzi kwa masonara na kwamba hawatakuwa na msalie mtume kwa masonara wanaofanya udanganyifu.

Amesema wameunda timu ambayo inafanya ukaguzi katika maduka yote ya masonara na kwamba hadi sasa kati ya maduka  21 waliyokagua wameyafungia maduka 6  kutokana na udanganyifu.

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani amewatoa wasiwasi wabunge kuwa Serikali inatekeleza miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo vyote.

Amesema hivi sasa kuna ziada ya umeme wa Megawati 148 za ziada na kwamba vyanzo vya umeme vinavyotokana na gesi vinatarajiwa kuzalisha 1045 Megawati katika miaka minne ijayo.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Adelardus Kilangi amesema wagawanya idara mbalimbali za kushughulikia mikataba ambazo ni pamoja na mikataba ya rasilimali, manunuzi na mikataba ya kimataifa ambapo pia kutakuwa na wabobezi katika idara hiyo.

Kuhusu kurejea mikataba, Dk Kilangi amesema wameshaanza kulifanyia kazi kwa kurejea mikataba ya Songas, utafutaji na uendelezaji wa petrol, gesi na mingine.