Mawaziri 15 wa SADC kuijadili DRC na Lesotho

Dk Augustine Mahiga

Muktasari:

Miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na kujadili hali ya kisiasa katika nchi za Lesotho na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Dar es Salaam. Taasisi ya Siasa, ulinzi na usalama ya SADC inayojumuisha mawaziri 15 kutoka nchi wanachama imekutana leo (Ijumaa)  jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Mwenyekiti wake, Dk Augustine Mahiga.

Miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na kujadili hali ya kisiasa katika nchi za Lesotho na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Akifungua mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Mahiga amesema mkutano huo utapokea pia taarifa ya kamati ndogo iliyokwenda kushughulikia mgogoro wa kisiasa nchini Congo.

Dk Mahiga amesema mawaziri hao pia watajadili maombi ya nchi za Burundi na Comoro kutaka kujiunga na SADC, kabla ya kupeleka ombi hilo kwenye mkutano mkuu wa wakuu wa nchi za Sadc.

"Katika kikao chetu, tutajadili pia namna ya kuwaenzi waasisi wa SADC, sambamba na kupanga tarehe moja ya kuadhimisha kumbukumbu ya ukombozi katika nchi zetu za SADC," amesema Dk Mahiga.