Mawaziri watano wamnadi mgombea wa CCM Monduli

Muktasari:

Mawaziri hao ni mbali na idadi ya wabunge 12 ambao tayari wamempigia kampeni mgombea huyo aliyehamia chama hicho tawala akitokea Chadema.

Monduli. Zikiwa zimebaki siku tano ufanyike uchaguzi mdogo, mawaziri watano tayari wamempigia kampeni mgombea wa CCM wa Jimbo la Monduli mkoani Arusha, Julius Kalanga.

Mawaziri hao ni mbali na idadi ya wabunge 12 ambao tayari wamempigia kampeni mgombea huyo aliyehamia chama hicho tawala akitokea Chadema.

Meneja wa kampeni za CCM katika jimbo hilo, William Ole Nasha siku kadhaa zilizopita alitangaza kuwa mgombea wao atapigiwa debe na wabunge 16 wa CCM.

Hata hivyo, hadi sasa wabunge wa CCM ambao wamekwisha fanya kampeni Monduli wako 17, hao ni pamoja na mawaziri na naibu mawaziri.

Mawaziri waliompigia debe Kalanga hadi jana ni Selemani Jafo (Tamisemi) na Dk Medard Kalemani (Nishati) na naibu mawaziri, Mussa Sima (Mazingira), Jumaa Aweso (Maji) na Ole Nasha (Elimu, Sayansi na Technolojia).

Wabunge waliokwenda Monduli hadi jana kupiga kampeni ni Sixtus Mapunda (Mbinga),Virajilai Jituson (Babati Vijijini), Catherine Magige (Viti maalumu), Dk Steven Kiruswa (Longido), Godluck Mlinga (Ulanga), Anna Lupembe (Katavi) na Esther Mahawe (Viti maalumu).

Wengine ni Joseph Kasheku maarufu Musukuma(Geita Vijijini), Martha Mlata (Viti maalumu), Fratei Massay (Mbulu Vijijini), Edwin Sanda (Kondoa Mjini) na Godwin Mollel (Siha).

Hoja za mawaziri na wabunge hao zilizungumzia zaidi kutatua kero za wananchi kwenye jimbo hilo, hasa migogoro ya ardhi na shida ya maji.

Waziri Jafo akizungumza kwenye mkutano wa kampeni wa Kata ya Naaralamii, aliwaeleza wananchi kuwa kero za maji na ardhi zimeanza kutatuliwa na mawaziri husika wa Maji na Umwagiliaji na yule wa Ardhi.

Alisema kuhusu tatizo la huduma za afya, Serikali inaendelea na mkakati wa ujenzi wa zahanati na vituo vya afya kwa kuwa fedha za dawa zimekwisha pelekwa katika wilaya hiyo.

Waziri Kalemani katika kata ya Lepurko, aliahidi Serikali itaendelea na mkakati wa kusambaza umeme vijijini hadi vijiji vyote vipate umeme wilayani humo.

Naibu Waziri Sima akizungumza katika mkutano wa kampeni wa Kata ya Makuyuni, alisema Serikali itazitatua kero za maji, mazingira na migogoro ya ardhi.

“Uchaguzi huu mnapaswa kuutumia kama fursa ya kubainisha kero zenu na kuomba zifanyiwe kazi,” alisema Sima.

Naibu Waziri Aweso aliahidi Serikali kuendelea kushughulikia matatizo ya maji katika wilaya hiyo, kwani tayari kuna miradi kadhaa inaendelea.

Ole Nasha, alisema Serikali itahakikisha watoto wote hasa wa jamii ya ufugaji wanakwenda shule, lakini pia kuendelea kuboresha miundo mbinu katika elimu.

Kuhusu wabunge alisema walisambazwa katika kata zote 16 za wilaya hiyo na wamezungumza na wananchi, kusikiliza kero zao na wameahidi Serikali itazifanyia kazi.

“Nimejipanga vizuri kimkakati kwenye kata kuna wabunge wote ambao wamejitolea kuhakikisha CCM inashinda, lakini pia tunafanya kampeni za kisasa zaidi kuzungumzia kero za wananchi na kutoa utatuzi tofauti na wenzetu wanaoomba kura ya heshima tu,” alisema.

Ole Nasha ambaye ni mbunge wa jimbo la Ngorongoro, alisema wananchi wa Monduli,

wametambua makosa waliyofanya mwaka 2015 na sasa watasahihisha.

“Mwitikio ni mkubwa katika mikutano yetu na wananchi wengi wanatuunga mkono, kwani tunafanya kampeni za kimkakati zaidi, kuzibainisha kero na kutoa ahadi ya kuzitekeleza tofauti na wenzetu ambao wanataka kura za kulinda heshima,” alisema.