Mawaziri watatu sasa kikaangoni kupinduka kwa Mv Nyerere

Muktasari:

Licha ya Rais John Magufuli kuchukua hatua kadhaa za kuvunja bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) huku Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Temesa, Dk Mussa Mgwatu watu wa kada mbalimbali wamesema hatua hiyo haitoshi, kutaka mawaziri watatu wajiuzulu.

Dar es Salaam. Ajali ya Kivuko cha Mv Nyerere wilayani Ukerewe kimeibua mambo mengi. Licha ya Rais John Magufuli kuivunja Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) na Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), bado watu wa kada mbalimbali wana shauku kuona hatua zaidi zikichukuliwa.

Kwa nyakati tofauti wanasiasa, wasomi na wananchi wa kawaida wamekuwa na maoni tofauti wakitaka mawaziri watatu na mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kuwajibika kwa kuwa ajali hiyo imetokea kwa madai ya uzembe unaozihusisha mamlaka zao za usimamizi.

Mawaziri ambao watu mbalimbali wanataka wawajibike ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe; Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama.

Kivuko cha Mv Nyerere kilipinduka Alhamisi iliyopita mita 50 kabla ya kutia nanga katika gati la kijiji cha Bwisya, Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 226.

Kupitia mitandao ya kijamii na mahojiano na Mwananchi, makundi hayo yanaonyesha kushangazwa na namna kazi ya uokoaji ilivyofanyika siku kilipopinduka kivuko hicho, uokoaji kusitishwa saa mbili usiku na kuendelea siku iliyofuata asubuhi kwa maelezo kuwa huenda watu wengi zaidi wangeokolewa wakiwa hai kama uokoaji usingesitishwa siku hiyo.

Pia, walirejea ajali mbalimbali za meli kuzama na namna ambavyo mamlaka husika zilivyoshindwa kujifunza na kuhakikisha kwa wananchi kuwa matukio hayo hayatajitokeza, au hata yakitokea athari haziwi kubwa.

Meli, ambayo ilizama na kuua watu wengi zaidi nchini ni Mv Bukoba mwaka 1996 ambapo zaidi ya watu 800 walifariki dunia.

Wakati hayo yakijadiliwa, jana taarifa ya mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa ilieleza kuwa Rais Magufuli ameivunja bodi ya Sumatra kutokana na kupinduka kwa kivuko hicho na ajali nyingine za barabarani zinazosababisha vifo, ulemavu na uharibifu wa mali.

Awali juzi, Rais alitangaza kuivunja bodi ya ushauri ya Temesa na kutengua uenyekiti wa Brigedia Jenerali mstaafu Mabula Mashauri wa Temesa kama alivyofanya kwa Dk John Ndunguru wa Sumatra.

Uwajibikaji

Akizungumzia uwajibikaji, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema kuwajibika kwa kiongozi ni jambo lililopo kisheria na kikatiba.

“Sheria inayoitwa Ministerial Responsibility (uwajibikaji wa majukumu ya kiwaziri) inalieleza wazi hili, kuwa kama kiongozi wa chini amefanya kitu kikaleta madhara kwa jamii, kama kilichofanyika kwenye Mv Nyerere kiongozi mkuu anapaswa kuwajibika kwa kujiuzulu,” alisema Henga.

“Sina shaka na hilo na wanaotoa maoni kumtaka waziri mwenye dhamana ajiuzulu wapo sahihi.”

Alifafanua: “Ndiyo maana Januari 22, 1977 aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo ambaye sasa ni Rais mstaafu (wa awamu ya pili), Ali Hassan Mwinyi alijiuzulu kutokana na kukithiri kwa mauaji ya vikongwe.”

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe licha ya kumpongeza Rais kwa kuvunja bodi, alienda mbali zaidi akitaka waziri ambaye bodi hizo zipo chini ya wizara yake kuwajibishwa.

“Hadi muda huu hakuna mtu aliyewasilisha barua ya kujiuzulu kutokana na tukio hili la meli kuzama (kupinduka),” alisema Zitto.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Zitto alisema: “Nchi zilizoendelea Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Waziri wa Ujenzi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu walitakiwa wawe wamekwishafutwa kazi au wamejiuzulu wenyewe.

“Ni wakati wa rafiki yangu Kangi Lugola kupumzika. Waziri Kamwelwe, Jenista na mkuu wa Mkoa wa Mwanza (Mongella) wanapaswa kufukuzwa kazi mara moja.”

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alihoji sababu za kuvunjwa kwa bodi ya ushauri na kuwaacha waliokuwa na mamlaka ya utendaji na sera.

Lissu alisema Temesa ipo chini ya mamlaka ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano hivyo waziri husika anapaswa kuchukuliwa hatua.

Mbunge huyo, ambaye yupo nchini Ubelgiji kwenye matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi Septemba mwaka jana akiwa bungeni jijini Dodoma, alikwenda mbali zaidi na kuhoji: “Mwaka 2016 tulipitisha sheria ya udhibiti wa majanga (Disaster management Act 2016) ambayo imekabidhi majukumu ya udhibiti wa majanga kwa waziri mkuu. Je, waziri mkuu na watendaji wake wanaohusika na majanga wamewajibishwaje kwa kushindwa kuokoa maisha ya waliokuwa kwenye kivuko cha Mv Nyerere?”

Naye Profesa George Shumbusho wa Chuo Kikuu cha Mzumbe alisema: “Nimejiuliza kwa nini bodi ivunjwe, waziri na katibu mkuu wabaki na sijapata jibu, kwa sababu kama ni suala la uwajibikaji wote wawajibike. Haina maana wamefanya wao, hapana! Wamefanya walio chini yao.”

Kuhusu kujiuzulu au kuwajibishwa katibu mkuu, Profesa Shumbusho alisema ni mtendaji wa Serikali hivyo waziri achukue dhamana ya kisiasa.

Alisema asipochukua hatua ya kisiasa akakaa pembeni ili kuonyesha ni kwa namna gani tukio hilo limemuumiza, aondolewe kwenye nafasi yake.

“Labda mheshimiwa Rais ameona ameondoa ondoa sana hivyo ameacha, hebu mtu ajifikirie mwenyewe,” alisema.

Alifafanua kuwa utamaduni wa kujiuzulu Tanzania haupo na kwamba huenda siku zijazo watendaji wataona umuhimu huo.

Wananchi watiririka

Wananchi mbalimbali wameendelea kutoa maoni yao kupitia mitandao ya kijamii ya kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), akiwamo James Butendeli aliyesema kuwa ni vizuri kuwavua madaraka.

Mchangiaji mwingine kwenye mtandao huo, Julius Labour aliandika kuwa kwa mtazamo wake hata waziri wa ulinzi hajasimamia vizuri, kwa sababu nchi ina jeshi la wanamaji ambao hawajafanya kitu.

Akitumia fumbo, Esmo Festo aliandika kuwa inawezekana alitakiwa achinje, lakini achinje ng’ombe, badala yake akachinja kuku wale waliojua alitakiwa kuchinja ambao ndiyo wengi wataona ameshachinja, ila wanaojua alitakiwa achinje nini ndiyo wataendelea kuhoji na kwa uchache wao hawatasikika.

Hata hivyo, Julius Nyang’ombe aliandika kuwa kama kivuko ni cha kubeba watu 110 (101) na kikabeba zaidi ya hapo ina maana usafiri ni shida, hivyo bila kuimarisha usafiri hata akiunda bodi mpya itakutana na yaleyale.

Mchangiaji mwingine, Khatemo Japhary aliandika kuwa ni mapema kumpongeza kwani waziri, naibu waziri, katibu mkuu, mkuu wa mkoa na watendaji lukuki wapo kwenye nafasi zao.

Hata hivyo, Elia 1757576262 aliandika: “Nchi hii historia ya kujiuzulu iliisha kwa Mwinyi msishangae kesho mpinzani akajiuzulu kuunga juhudi, hili likasahaulika akili za Watanzania ziko jirani na ... ni wepesi kusahau.”