VIDEO-Mawaziri wawili ‘watema cheche’ bungeni

Muktasari:

Wajibu hoja za wabunge waliochangia taarifa za utekelezaji wa shughuli za kamati mbili za Kilimo, Mifugo na Maji na ile ya Ardhi, Maliasili na Utalii, mawaziri hao walisema wataendelea kufanya kazi zao kwa weledi bila woga wa kumshughulikia mtu yeyote anayekwenda kinyume cha sheria.

 Mawaziri wawili, Luhaga Mpina na Dk Hamisi Kigwangalla ‘wametema cheche’ jana bungeni walipokuwa wakijibu hoja za wabunge kuhusu utendaji wao.

Wajibu hoja za wabunge waliochangia taarifa za utekelezaji wa shughuli za kamati mbili za Kilimo, Mifugo na Maji na ile ya Ardhi, Maliasili na Utalii, mawaziri hao walisema wataendelea kufanya kazi zao kwa weledi bila woga wa kumshughulikia mtu yeyote anayekwenda kinyume cha sheria.

Mpina ambaye ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, alisema ataendelea kuwashughulikia wote bila kujali mtu hata kama ni baba yake mzazi.

Alisema vita ya kupambana na uvuvi haramu imekuwa ngumu kwake kutokana na kuwa inawashirikisha baadhi ya wabunge ambao aliahidi kuwa wakati wowote atawataja kwa kuwa hana hofu.

Alisema operesheni aliyoianzisha haina mwisho na kuwa anafanya kazi yake kama kibarua lakini wenye mali ni watanzania.

Dk Kigwangalla anayesimamia Wizara ya Maliasili na Utalii, alisema hana hofu kwa kuwa mamlaka ya uteuzi ilizingatia kuwateua watu ambao ni weledi na wanaoweza kulisaidia taifa. Alisema sekta yake inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo kuvamiwa kwa maeneo yake hasa kwenye hifadhi.

Majibu ya mawaziri hao yametokana na hoja mbalimbali zilizoelekezwa kwao katika michango ya wabunge.

Mbunge wa Busega (CCM), Dk Raphael Chegeni alisema Mpina anakuwa na kiburi na kumtaka aache kwa kuwa anawaumiza wafugaji. “Kamata kamata ya mifugo inawaumiza wafugaji, wewe waziri unatoka Kanda ya Ziwa ambako kuna mifugo mingi zaidi na wewe waziri unatoka eneo hilo lakini hivi unataka tulie humu ndani au, ni aibu hiyo.”

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye alisema hakuna lililofanyika kwa wafugaji tangu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ulipomalizika, “Mwaka 2013/14 na 2015 nilizunguka nchi nzima nikizungumza na wafugaji na nilitegemea baada ya Uchaguzi Mkuu hali zao zingekuwa afadhali, lakini zimekuwa mbaya tena mbaya zaidi kuliko ilivyo kuwa mwanzo, tukubali kuwa Serikali tumeshindwa kuwasaidia wafugaji,” alisema Nape.

Alisema kila wakati Serikali inafanya kazi ya zimamoto badala ya kujipanga na kushughulikia matatizo ya wananchi kikamilifu hivyo, alipendekeza kuundwa kamati maalumu kuangalia namna bora ya kushughulikia matatizo ya wafugaji.

Alisema mifugo imekuwa ikishikiliwa bila hata sababu za msingi huku mingine ikifa. “Kwa mfano, Meatu kuna ng’ombe 948 wanashikiliwa, Kakonko (700), Bukombe (716), Kasulu (90), Chemba (411), Mlele (640) na Kaliua (1,129),” alisema.

Alisema baadhi ya mifugo inakufa kwa kupigwa risasi na kukosa huduma akitoa mfano kwamba, Katavi mwaka 2015/18, ng’ombe 6,503 walikufa, Bunda (150), Morogoro (200), Meatu (148) na Chemba (196).

Mbunge wa Simanjiro (Chadema), James ole Milya alisema, juzi Mahakama ya Wilaya ya Same ilitaifisha ng’ombe 36 na maeneo mengine wafugaji wanaendelea kuumizwa hivyo kushauri iundwe kamati ya uchunguzi.

Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma alizungumzia ukamataji wa nyavu za uvuvi akisema anatoa rai kwa mawaziri kama Mpina wapunguze mihemko kwa kuwa hata wao wanatamani kuendelea kuwa wabunge.

Alisema jimboni kwake na maeneo mengine ya kanda ya Ziwa debe la dagaa linauzwa Sh50,000 ikiwa na maana hata dagaa hawawezi kula.

“Namuomba Mpina atakapokuja hapa atueleze ni sheria gani anazozitumia kwa sababu Rais Magufuli alikuwa waziri (kwenye wizara hiyo) kabla ya kuwa Rais lakini yeye aliunda BMU, watu wakawa wanafundishwa kukawa hakuna uvuvi haramu,” alisema.

Alishauri iundwe tume kuchunguza iwapo fedha za faini wanazotozwa wavuvi hukatiwa risiti za Serikali.

Waziri wa Maliasili

Mbunge wa Chambani (CUF), Yusuph Salum Hussein, alisema Wizara ya Maliasili na Utalii ni kama yai viza ambalo lina matumizi mazuri kwa wanaolitumia lakini likikosewa linanuka.

“Nikushauri (waziri Dk Kigwangalla) uwe mtulivu, hii wizara haitaki amri, haitaki nguvu, haitaki ubabe, haitaki hasira, hii wizara ni lazima utulie na sisi tunawashauri watu humu ndani. Ndani ya wizara hii lazima mafiga matatu,” alisema.

Aliyataja mafiga hayo kuwa ni jamii, Serikali na wawekezaji akisema wanalazimika kukaa pamoja.

“Kwa hiyo lazima utulie vizuri sana hizi figa tatu zikae... Vinginevyo utakuwa ni waziri ambaye umetumikia wizara hii kwa muda mfupi sana. Na kwa sababu imebeba uchumi wetu, ukivuruga katika sekta hii kidogo tu, unaharibu uchumi wa nchi,” alisema.

Mbunge wa Iringa Mjini, (Chadema) Mchungaji Peter Msigwa alisema Kamati ya Maliasili imepokea malalamiko kutokana na hatua ya waziri kufuta vitalu vya uwindaji.

“Leo waziri anasema anafuta hizi leseni, naomba nimshauri, kuna vitalu 61 ambavyo havina watu kama angetaka vifanyiwe minada anayoitaka, angeanza na hivyo ambavyo havina watu hadi sasa huko porini,” alisema.

“Nimshauri waziri hii tasnia anatakiwa achukue muda kuisoma, binafsi nimefanikiwa kwenda kwenye maeneo ambayo nimeona wamewekeza hao wawekezaji kwa hiyo tukianza kuvuruga kwa mihemko haitatusaidia,” alisema.

“Serikali tumekuwa tukiilaumu kila mtu anafanya kazi kivyake, sasa tasnia hii, utalii huu umejengwa kwa muda mrefu sana na akitokea mtu mmoja anayetaka umaarufu atauvuruga kwa muda mfupi sana,” alisema.

“Huyuhuyu waziri anatoa amri anapingana na Waziri wa Ardhi, huyohuyo mmoja anapingana na Waziri wa Uvuvi. Hatuwezi kuwa na mawaziri wanaofanya kazi kwa mizuka, tunataka Taifa letu tufanye kazi kwa kupendana na kuheshimiana na ndiyo maana nimesema hamjajipanga vipaumbele vya nchi hii ni vipi.

“Kila mtu akiamka asubuhi ana mzuka wake, anabeba waandishi wa habari wanabeba na makamera akasema anayoyataka ndiyo maana nimesema Waziri Mkuu anatakiwa awe hapa,” alisema Msigwa.

Lukuvi, Kamwelwe w ajibu hoja

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alieleza mikakati ya kurasimisha majengo katika maeneo yaliyojengwa kiholela bila kusumbuliwa.

Kauli ya waziri hiyo ilipokewa kwa shangwe na wabunge wengi kwa kupiga makofi huku mbunge Msukuma akitaka mawaziri wengine kuiga mfano wa waziri huyo.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isaak Kamwelwe aliahidi kutolea ufaganuzi maeneo yote yanayotakiwa kupatiwa maji na akwamba atawakabidhi wabunge kabla ya ijumaa.

Hata hivyo, hamu ya wabunge hasa wanaotoka katika ukanda wa kilimo cha mahindi waliotaka kujua mkakati wa Serikali wa kuongeza bei ya mahindi haikukatwa baada ya Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tzeba kuweka msimamo kuwa mazao hayo yanasimamiwa kwa mujibu wa sheria hivyo ni ngumu kufungua mipaka bila tafiti.