Maxmalipo yataja sababu abiria mwendokasi kusafiri bure

Muktasari:

Mkurugenzi wa kampuni hiyo alisema kwamba tatizo ni Udart kutowalipa fedha


Dodoma. Kampuni ya Maxmalipo Africa PLC imewaeleza wabunge chanzo cha abiria wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam kusafiri bure pamoja na ufanisi wa mradi huo kwa siku za usoni.

Kampuni hiyo imesema hayo leo Juni 19, 2018 wakati wa semina ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu iliyofanyika Ukumbi wa Msekwa, bungeni jijini Dodoma.

Mwanzishi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Maxmalipo, Mhandisi Juma Rajabu amesema kilichojitokeza hadi abiria wakasafiri bure ni baada ya watoa huduma Udart kushindwa kuwalipa fedha walizokuwa wanadai.

“Utaratibu ulikuwa kila tarehe 20 watoa huduma ambao ni Udart walipaswa kutulipa fedha ambazo nasi tunawalipa wafanyakazi wetu. Lakini hawakuwa wanafanya hivyo na sisi tukawa tunachukua fedha sehemu nyingine tunawalipa wafanyakazi,” amesema Rajabu na kuongeza:

“Ilifika mahali tukafungua kesi mahakamani, lakini Serikali ikatueleze inalishughulikia, lakini siku ya mgomo wafanyakazi wale walikuwa hawajalipwa miezi mitatu ndiyo maana waligoma, kwa hiyo tukawaeleza Udart watulipe na walipotulipa tu huduma zikarejea kwa abiria kulipa nauli.”

Kuhusu msongamano wa abiria, Rajabu amesema kwa kuwa mradi huo unapaswa kuwa na magari 305 lakini kwa sasa kuna magari 140 kati yake 39 ni makubwa.

“Kwa hiyo kama magari yote 305 yataingia, basi tatizo halitokuwapo. Pia katika vituo vyote, milango itafunguliwa na kutoa huduma tofauti na sasa ambapo baadhi vinatoa upande mmoja wa mlango na mwingine umefungwa,” amesema.