May aiambia EU: Uingereza inataka heshima

Waziri Mkuu Theresa May

Muktasari:

Waziri Mkuu May aliyezungumza siku moja baada ya kurudi kutoka kwenye mkutano huo wa kilele uliofanyika Salzburg, Austria aliitaka EU kuondoa vikwazo vyake katika mpango wake au waje na mpango mbadala.

London, Uingereza. Waziri Mkuu Theresa May Ijumaa alisema kuwa mazungumzo na Umoja wa Ulaya (EU) "yalikuwa shida kubwa" baada ya mkutano wa kilele ambapo mpango wake wa kujitoa EU mchakato unaofahamika kama Brexit ulikataliwa kwa kiasi kikubwa.
May akitumia sauti kali ya msisistizo wakati akitoa taarifa ya mazungumzo hayo Downing Street aliomba Umoja wa Ulaya "kuheshimu" msimamo wa Uingereza na matokeo ya kura ya maoni iliyofanyika Juni 2016.
Waziri Mkuu May aliyezungumza siku moja baada ya kurudi kutoka kwenye mkutano huo wa kilele uliofanyika Salzburg, Austria aliitaka EU kuondoa vikwazo vyake katika mpango wake au waje na mpango mbadala.
"Katika mchakato huu, nimeitendea EU kwa heshima. Uingereza inatarajia mambo kama hayo. Uhusiano mzuri mwishoni mwa mchakato huu unategemea hicho," alisema.
Ikulu ya Downing Street ilikuwa na matumaini kuwa mkutano huo wa kilele wa Salzburg usio rasmi ungewapa utatuzi unaoeleweka juu ya masuala katika majadiliano ya Brexit kabla ya mkutano rasmi Oktoba. Badala yake, viongozi wa mataifa 27 yaliyobaki ya EU bila kutarajia walikuwa na msimamo kinzani kwa mapendekezo yake.
Viongozi wa EU Alhamisi walisema kuwa mwezi ujao watashinikiza juu ya kupatikana mwafaka wa Uingereza kujiondoa katika umoja huo, lakini walimwonya May kuwa ikiwa hatalegeza msimamo kuhusu masuala ya biashara na mpaka wa Ireland ifikapo Novemba basi wako tayari kukabiliana na hali itakavyokuwa hata pale Uingereza itakapojiondoa.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya, Jean-Claude Juncker alisema baada ya mkutano wa kilele wa siku mbili mjini Salzburg Austria kuwa watu wa UIaya wana mipango kamili ya kuzingatia ikiwa hapatakuwa na makubaliano kabla ya Uingereza kujiondoa mwezi Machi mwakani.
May ameahidi kuwasilisha mapendekezo mapya kuhusu suala la biashara na Umoja wa Ulaya, yanayolenga pia kutatua hoja kuhusu mipaka ya Ireland Kaskazini akisema kuwa ndio njia pekee ya kusonga mbele.