Mazishi ya kitaifa Ukara

Askari wa mgambo wakiwa wamebeba majeneza yenye miili ya watu walifariki katika ajali ya kivuko cha Mv Nyerere baada ya kufikishwa katika makaburi eneo la Bwisya, Ukara mkoani Mwanza jana. Picha na Michael Jamson

Muktasari:

  • Ibada ya mazishi hayo yaliyohudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ilianza asubuhi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wanasiasa na wananchi, ilifanyika katika makaburi yaliyo umbali kwa takribani mita 100 kutoka mahali kilipozama kivuko hicho.

Dar es Salaam. Vilio, majonzi na simanzi jana vilitawala katika viwanja vya Shule ya Sekondari Bwisya, Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe jana wakati wa mazishi ya kitaifa ya baadhi ya watu waliokufa katika ajali ya kivuko cha Mv Nyerere.

Ibada ya mazishi hayo yaliyohudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ilianza asubuhi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wanasiasa na wananchi, ilifanyika katika makaburi yaliyo umbali kwa takribani mita 100 kutoka mahali kilipozama kivuko hicho.

Kabla ya kuanza kwa ibada hiyo, viongozi mbalimbali walitoa salamu za rambirambi huku Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe akitoa taarifa za ajali hiyo na kueleza kuwa licha ya kuwa na uwezo wa kubeba abiria 101, kivuko hicho kilikuwa kimepakia abiria zaidi ya 265.

Pia alitoa mchanganuo wa vifo hivyo na kubainisha kuwa wanawake ni 126, wanaume 71, watoto wa kike 17, watoto wa kiume 10 ambao jumla yao hadi wakati wa mazishi mchana ilikuwa 224.

Alisema miili 219 iliyotambuliwa ilichukuliwa na ndugu hadi saa tisa alasiri jana huku miili mingine mitano ikiwa haijatambuliwa.

“Miili hii ambayo haijatambuliwa imechukuliwa kipimo cha (utambuzi wa vinasaba) DNA ili ndugu zao watakapofika waweze kutambua kuwa wamepoteza ndugu,” alisema Kamwelwe.

“Miili mingine mitano iliyotambuliwa ndugu zao waliamua kuungana nasi katika mazishi haya. Hivyo leo itazikwa miili tisa.”

Uokoaji ulivyokuwa

Alisema ajali hiyo ilitokea Alhamisi iliyopita saa 7:48 mchana na ilipofika saa 8.10 mchana taarifa zilifika kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella aliyekuwa katika kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa.

Alisema saa 10 jioni, Mongella na kamati hiyo waliwasili eneo la tukio na kukuta wananchi wakiwa wameshaokoa watu 40.

Kuhusu michango inayotolewa, alisema mpaka jana fedha zilizokuwa zimechangwa na wananchi kwa ajili ya kusaidia shughuli hiyo ni Sh240 milioni.

Vivuko kununuliwa

Waziri huyo pia alitoa ahadi akisema, “Serikali iko katika mpango wa kununua vivuko salama ili wananchi waweze kuendelea na shughuli za kiuchumi.”

Ahadi ya kivuko pia ilitolewa na Waziri Mkuu ambaye alisema katika kuhakikisha wananchi wa eneo hilo hawapati adha ya usafiri katika kipindi hiki, Serikali iko katika mkakati wa kuwapelekea kivuko cha muda ambacho ni boti ya Serikali huku ikiendelea kufanya mazungumzo juu ya matumizi ya meli ya Mv Nyehunge.

“Pia tutafanya ukarabati wa kutosha katika baadhi ya vivuko ikiwamo Mv Misungwi na Sengerema ili kuimarisha usafiri wa majini katika maeneo yote,” alisema Majaliwa.

Wahusika wakamatwa

Akizungumzia watu wanaodaiwa kuhusika na kuzama kwa kivuko hicho, Majaliwa alisema, “Tayari tumeanza kuwakamata wote wanaohusika na uendeshaji wa vivuko na wenye wajibu wa kusimamia usalama wa vyombo vya majini kwa mahojiano ya awali na muda wowote kuanzia sasa, tume ya uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali itatangazwa.”

Majaliwa aliwataka Watanzania kuendelea kuwatia moyo wafiwa badala ya kutamka maneno yanayoweza kujenga chuki.

“Watu hawa wamepoteza ndugu zao wa muhimu hivyo ni vyema kuwapatia maneno mazuri yanayotia moyo badala ya kuwajaza maneno ya upotoshaji na tuiache Serikali ifanye jitihada zake,” alisema Majaliwa.

Matumizi fedha zinazochangwa

Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwatoa hofu Watanzania wanaoendelea kuchangia waathirika kwa maelezo kuwa fedha hizo hazitatumika katika shughuli nyingine tofauti na hiyo kwa sababu ni kwa ajili ya wafiwa.

“Baadhi ya pesa zitakazopatikana katika michango hiyo, zitatumika kujenga uzio katika makaburi haya na nyingine zitatumika kujenga mnara kama kumbukumbu katika eneo hili,” alisema Majaliwa.

Uopoaji wa miili

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama alisema baada ya mazishi hayo kazi ya kuhakikisha miili yote inaopolewa itaendelea.

“Lazima tuhakikishe pia imetambulika, imezikwa lakini hata ile ambayo haijatambuliwa inahifadhiwa na kwa upande wa wizara ya uchukuzi, wahakikishe kivuko chetu kinarudishwa nchi kavu na kufanyiwa matengenezo,” alisema.

Aidha, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humprey Polepole alisema chama hicho tawala kitaendelea kuisimamia Serikali kuhakikisha miundombinu ya usafirishaji katika Ziwa Victoria inaimarika na kuweka sheria za kusimamia uendeshwaji wa vyombo vya majini.

Polepole alisema chama hicho hakipo tayari kuona nguvu kazi inaendelea kupotea kwa vitu vinavyoweza kuzuilika.

“Sote tumejawa na simanzi lakini tunamuomba Mungu aweze kuwapa nguvu wafiwa katika kipindi hiki kigumu,” alisema Polepole.

Mbunge aomba kivuko kingine

Awali, katika salamu zake, Mbunge wa Ukerewe, Joseph Mkundi aliiomba Serikali kutafuta namna ili wakazi wa maeneo hayo wapate kivuko kingine cha kuwaunganisha.

“Hii ndiyo namna pekee ya kutufariji kwa msiba huu mkubwa uliotukumba,” alisema Mkundi.

Alisema licha ya ajali hiyo maisha ya wakazi wa Ukara ya kuvuka kwenda Bugolora kufuata mahitaji lazima yaendelee.

Ombi kama hilo lilitoka kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, George Nyamaha ambaye pia aliiomba Serikali kuimarisha utendaji wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) wilayani Ukerewe kwa kuipa vifaa, zana na nguvu kazi ili imudu kutekeleza na kusimamia usalama wa wasafiri.

“Sumatra ina mtumishi mmoja pekee wilayani Ukerewe, tena asiye hata na usafiri. Hawezi kutekeleza majukumu yake ipasavyo katika visiwa 38 vya wilaya hii,” alisema Nyamaha.

Salamu za Dk Shein

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed, akisoma salamu za rambirambi kutoka kwa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein, alisema msiba huo umegusa wengi na kuwaombea majeruhi wapone haraka.

“Tunawashukuru na kuwapongeza watu wote walioshiriki katika shughuli hili wakiwamo waokoaji, askari pia wahudumu wa afya wanaoendelea kutoa huduma kwa majeruhi,” alisema Mohammed

Awali, Mongella aliwapongeza wananchi, wakazi na wavuvi wa Ukara kwa kujitolea kufanya kazi ya uokoaji tangu ilipotokea ajali hiyo hadi timu ya mkoa ilipowasili saa 10:45 alasiri ambako tayari watu 40 walikuwa wameokolewa.

“Wavuvi wa Kijiji cha Bwisya na kisiwa kizima cha Ukara wamejitolea bure boti zao za uvuvi wakipeana zamu kuopoa maiti. Ni vigumu kumshukuru mtu mmojammoja. Serikali ya mkoa inamshukuru kila mtu kwa nafasi yake,” alisema Mongella.