Mazito aliyoshuhudia Majaliwa ziarani

Muktasari:

Majaliwa alifanya ziara ya siku saba katika wilaya saba zenye halmashauri nane mkoani Mwanza.

Kero za maji, migogoro ya ardhi, ya wenyeviti, madiwani, meya, watumishi na wakurugenzi wa halmashauri ni miongoni mwa mambo yaliyojitokeza wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Majaliwa alifanya ziara ya siku saba katika wilaya saba zenye halmashauri nane mkoani Mwanza.

Alianza ziara Februari 14 katika Halmashauri ya Buchosa iliyopo wilayani Sengerema na kumaliza Februari 21 wilayani Nyamagana alikokutana na wadau wa pamba ambao pamoja na mambo mengine walijadili kuanza kwa msimu, mfumo wa uzalishaji na ununuzi.

Wilaya nyingine za mkoa huo ni Kwimba, Magu, Ukerewe, Misungwi na Ilemela.

Kero kila mahali

Katika ziara hiyo alibaini halmashauri nyingi kuwa na migawanyiko baina ya wakurugenzi, meya, wenyeviti, madiwani na watumishi kutokana na masilahi binafsi.

Akiwa wilayani Misungwi, Majaliwa alimsimamisha kazi mwanasheria wa halmashauri hiyo, Alphonce Sebukoto kwa kuisababishia hasara ya Sh138 milioni kutokana na kushindwa kuishauri vyema na kuidhinisha Sh279 milioni zilipwe kwa mwenyekiti wa halmashauri, Anthony Bahebe kupitia akaunti yake binafsi.

Bahebe aliishtaki halmashauri akitaka alipwe fedha hizo ikiwa ni malipo ya utekelezaji wa mradi wa maji katika Kijiji cha Igenge uliofanywa na kampuni ya Seekevim.

Akizungumza na watumishi wa halmashauri hiyo, Majaliwa aliagiza watu hao wachunguzwe na tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imewatia mbaroni.

Akiwa wilayani Kwimba wananchi walisimamisha msafara wake wakiwa na mabango mengi ya kumkataa mkuu wa wilaya hiyo, Mtemi Msafiri wakidai anawanyanyasa. Miongoni mwa unyanyasaji walisema ni pamoja na kuwakamata kwa kisingizio cha uzururaji kisha kuwapeleka kwenye shamba lake binafsi kufanya kazi za kilimo, huku akizuia magari makubwa kuingia na kutoka kwa ajili ya kuchukua mazao.

Majaliwa aliwataka wakusanye mabango yote yaliyokuwa yameandikwa kumkataa mkuu huyo wa wilaya na kumwagiza msaidizi wake ayachukue na kuyaweka kwenye gari akisema, “hapa kuna jambo lazima tuwasikilize.”

Baada ya hapo aliwatuliza na kuahidi kuwa yatafanyiwa kazi, hata hivyo alikemea kitendo hicho akidai wapo madiwani walioandaa jambo hilo akisema msafara huo upo kisheria hivyo kuingilia katikati kwa kuandaliwa lolote linaweza kutokea, “tuache haya mambo kitendo hiki hakipendezi.

Kwa upande wake, Mtemi alisema watu wameandaliwa kwa kupewa fedha kumchafua. Akiwa kwenye kikao na watumishi wa halmashauri hiyo, Majaliwa alimjia juu Mkurugenzi mtendaji, Pendo Malabeja akidai tangu ateuliwe kufanya kazi katika halmashauri hiyo mwaka 2012 hakuna maendeleo yoyote yaliyopatikana badala yake fedha za maendeleo zinazopelekwa hazionekani.

“Wewe mkurugenzi ndiye mtendaji na msimamizi mkuu wa halmashauri, fedha nyingi zinazoletwa hapa kwa ajili ya maendeleo hazionekani, miradi haitekelezwi kumalizika, lakini fedha zenyewe hazijulikani zimeenda wapi. Hatuwezi kuvumilia fedha za Serikali ziendelee kupotea,” alisema.

“Kwa kuwa sote ni wateuliwa, jambo hili naondoka nalo ila majibu tutayapata baadaye.”

Majaliwa alitoa kibano tena kwa Mkurugenzi mtendaji wa Ukerewe, Frank Bahati na Mweka hazina wake, Peter Molleli kwa kuwapa saa 72 kumpatia maelezo ya kina kuhusu zilipo zaidi ya Sh340 milioni zilizopelekwa kwa ajili ya maendeleo.

Alisema Serikali ilipeleka Sh451 milioni za maendeleo (CDG), kati ya hizo Sh221 milioni hazionekanai zilipo, nyingine Sh65 milioni zilipelekwa kwa ajili ya mradi wa umwagiliaji Bugolola nazo hazionekani huku Sh23 milioni kati ya Sh84 milioni za motisha kwa walimu na Sh37 milioni za madai ya watumishi hazijulikani zilipo.

Licha ya kusema anataka majibu ya fedha hizo Februari 21 wakati wa tathmini ya ziara yake hakuzungumza chochote.

Aagiza wawili wakamatwe

Akiwa katika Halmashauri ya Buchosa, Majaliwa aliagiza wakandarasi watatu wanaotekeleza miradi ya maji kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuitekeleza chini ya viwango ikiwa na gharama ya zaidi ya Sh4 bilioni.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya baadhi ya madiwani na Mbunge wa jimbo, Dk Charles Tizeba kutoa malalamiko yao wakidai miradi hiyo ilianza kutekelezwa mwaka 2012, lakini imekuwa ikisuasua huku mabomba yanayotandazwa hayakidhi viwango yanapasuka.

Diwani wa Kalebezo, Charles Kishinja alisema hali ni mbaya kwa wananchi licha ya miradi hiyo kutengewa fedha nyingi.

Hali ilikuwa mbaya zaidi Majaliwa alipomtaka mhandisi wa maji wa wilaya hiyo kutoa ufafanuzi kuhusu madai hayo na Kaimu mhandisi, Maghembe Makara kusema maji yanatoka ndipo Dk Tizeba aliposimama na kumnanga.

“Haya anayoyasema ni uongo mtupu hakuna maji, kwa kweli hali ni mbaya nashangaa kuona kauli hizi na tatizo hili lilianzia kwa mkandarasi mshauri na hata msanifu walikuwa wote wabovu. Hatuna mradi hapa, tunatakiwa tupate miradi mipya,” alisema Tizeba.

Miradi hiyo inatekelezwa na wakandarasi watatu tofauti ambao ni Pet Cooparation anayetekeleza mradi wa Lumeya, Kalebezo na Nyehunge kwa gharama ya Sh1.4 bilioni. Mwingine ni Luneco Investiment wa mradi wa Lumeya, Nyakalilo hadi Bukokwa kwa gharama ya Sh1.4 bilioni.

Mkandarasi mwingine ni Memo co Ltd anayetekeleza mradi wa Luchili, Nyakasungwa na Igwanzozu kwa gharama Sh1.7 bilioni.

Baada ya Tizeba kusema hivyo Majaliwa alimtaka Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Ernest Madale kutoa ufafanuzi nini wamefanya dhidi ya wakandarasi hao ambapo alisema tatizo kubwa lipo kwa mkurugenzi wa mashtaka (DPP) kuchelewesha kurudisha mafaili.

Baada ya kauli hiyo, Majaliwa alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella baada ya ziara hiyo kuwasiliana na ofisi ya DPP kushughulikia haraka majalada hayo ili kuharakisha kesi zao.

Kauli kama hiyo ya kukamatwa kwa wakandarasi na kuwafikisha mahakamani aliitoa pia akiwa katika Kijiji cha Lumambogo wilayani Kwimba alipotaka asakwe mkandarasi wa kampuni ya Palemo aliyetelekeza mradi wa maji wa Sh2.9 bilioni ulioanza tangu mwaka 2013 kwa ajili ya vijiji vinane.

Majaliwa alitoa kauli hiyo baada ya kuzindua mradi wa maji wa thamani ya Sh630 milioni utakaohudumia wakazi 15,670 na kuagiza kuharakisha taratibu za kuvunja mkataba na mkanadarasi huyo.

Mhandisi wa maji wa Halmashauri ya Kwimba, Philip Boaz wakati akitoa ufafanuzi kuhusu mradi huo, alisema wameshaanza kuchukua hatua dhidi ya mkandarasi huyo za kumtaka arejeshe fedha na amesharejesha Sh184 milioni kati ya Sh412 milioni alizokuwa ameshapewa.

Migogoro ya watumishi

Katika ziara hiyo Majaliwa alikemea migogoro aliyoikuta kati ya wakurugenzi, wenyeviti wa halmashauri, madiwani na watendaji akidai inarudisha nyuma maendeleo.

Halmashauri alizokuta zina migogoro ya watumishi ni Ilemela, Kwimba, Misungwi, Buchosa, Ukerewe na Nyamagana ambayo yote kwa pamoja alisema inatokana na masilahi binafsi huku watendaji wakidharau madiwani.

Katika mgogoro wa halmshauri ya Misungwi, mbunge wa jimbo hilo, Charles Kitwanga alimkataa mkurugenzi mbele ya waziri mkuu akidai hafai kuendelea kufanya kazi eneo hilo kwa kuwa anaibua migogoro na mbadhirifu wa fedha.

Akiwa Manispaa ya Ilemela, Majaliwa alimbana mkurugenzi wake, John Wanga akitaka kujua lini watawalipa fedha wananchi wa Mhonze waliofanyiwa thamani muda mrefu, lakini hawalipwi. Hata hivyo, Wanga alikosa majibu na ndipo mkuu wa mkoa akaokoa jahazi kwa kuahidi kuwa jambo hilo litatafutiwa ufumbuzi.