Mbatia alia rafu chaguzi ndogo

Muktasari:

Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo, alidai matukio ya vurugu na matumizi ya nguvu ya polisi dhidi ya viongozi, wafuasi wa upinzani na baadhi ya wananchi huko Tarime hayakubaliki.

Moshi. Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ameisihi Serikali kuendesha nchi kwa misingi ya utawala bora inayoheshimu utawala wa sheria ili kuepusha chuki kuota mizizi nchini.

Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo, alidai matukio ya vurugu na matumizi ya nguvu ya polisi dhidi ya viongozi, wafuasi wa upinzani na baadhi ya wananchi huko Tarime hayakubaliki.

Juzi polisi walivunja mkutano wa hadhara katika kata ya Turwa wa kumnadi mgombea wa Chadema, ambapo polisi wanadaiwa kutumia mabomu ya machozi kutawanya watu na kumkamata Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko na watu wengine zaidi ya 20.

“Ukiweka utaratibu na usiufuate ni vurugu. Shughuli za kampeni za uchaguzi wowote zimewekwa kisheria. Ubabe unaoendelea unazidisha chuki badala ya kujenga taifa,” alisema.

“Tukiendelea kukiuka sheria hivi, iko siku Watanzania watafanya jambo ambalo halikutegemewa. Tusiendeshe nchi kwa mihemko na ubaguzi na baadhi kujiona bora kuliko wengine,” alisisitiza.

“Leo mnafanya figisufigisu ili wabunge na madiwani wahamie CCM lakini mjue Watanzania wanawatazama. Yana mwisho haya.”

Wakati huohuo, Kaimu Mwenyekiti wa Chadema mkoa Kilimanjaro, Joseph Selasini amewataka makachero wa Polisi kuacha kujificha na kurekodi kwa siri mikutano ya kampeni ya chama hicho.

Akihutubia mikutano ya kumnadi mgombea udiwani kata ya Mawenzi Moshi mjini kwa tiketi ya Chadema, Afrikana Mlay, Selasini alisema kamwe hawataogopa kukosoa hata kama wanarekodiwa.

“Tunawasihi sana polisi. Fanyeni kazi yenu ya kulinda usalama wa raia na mali zao. Hii kazi ya kujificha na kuturekodi si yenu,” alisema.

Katika mkutano uliofanyika eneo la Tanesco Moshi, Selasini alienda mbali na kumtaja askari mmoja kwa jina na kumtaka aache kurekodi hotuba zao kwa siri, bali afike mbele arekodi kwa amani.

Akihutubia mkutano huo, Mbunge wa Jimbo la Moshi mjini, Jaffar Michael, aliwasihi wananchi wa kata hiyo kumchagua Mlay, ili washirikiane kuhakikisha Moshi inakuwa Jiji kabla ya 2020.