Mbegu bora za chai, kahawa kuwatajirisha wakulima

Muktasari:

  • Kuongezeka kwa mavuno kutapandisha kipato cha wakulima hao, hivyo kuwapa nafasi ya kutumia fursa za kujenga viwanda vidogo vitakavyoongeza thamani ya mazao yao na kuleta mapinduzi kwenye sekta hiyo inayotoa ajiri kwa zaidi ya asilimia 80 nchini.

 Wakulima wanatarajia kunufaika na kazi za mikono yao baada ya kupatikana kwa mbegu zinazovumilia ukame na magonjwa, jambo litakaloongeza mavuno.

Kuongezeka kwa mavuno kutapandisha kipato cha wakulima hao, hivyo kuwapa nafasi ya kutumia fursa za kujenga viwanda vidogo vitakavyoongeza thamani ya mazao yao na kuleta mapinduzi kwenye sekta hiyo inayotoa ajiri kwa zaidi ya asilimia 80 nchini.

Kupitia Mpango wa Kusaidia Biashara na Kilimo (TASP) unaofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya, Taasisi ya Utafiti wa Chai (Trit), inasema imefanikiwa kuzalisha aina nne za miche ya chai itakayoongeza tija kwa mkulima. Pia, imefanikiwa kuwaunganisha wakulima na kujenga ghala la pembejeo Wilayani Mufindi linalohudumia zaidi ya wakulima 1,200.

Mkurugenzi Mtendaji wa Trit, Dk Emmanuel Simbua akizungumza na Gazeti hili hivi karibuni, alisema vituo 20 vya kupimia hali ya hewa vimewekwa katika maeneo yanayozalisha chai ili kuwasaidia wakulima.

Hata hivyo, alisema bado kuna changamoto zinazowakabili wakulima wadogo wanaowalea.

Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (Tacri), imesema imefanikiwa kuendeleza aina 23 za mbegu inayoongeza mavuno na kupunguza gharama za viatilifu kwa asilimia 50.

Katika utekelezaji wake, Tacri imewafikia zaidi ya wakulima 4,000 iliyowapa mafunzo ya kilimo cha kisasa.

Taarifa ya Tacri inasema imefanya tathmini ya kuvumilia athari za ukame na matokeo yanayotarajiwa kukamilika mwaka ujao wa fedha.

Chai na kahawa ni miongoni mwa mazao yanayoliingizia Taifa fedha za kigeni. Hata hivyo, mazao haya yamekuwa yakikabiliwa na ukame na magonjwa ambayo yanaathiri ubora wake.

Umoja wa Ulaya ulisaidia taasisi za utafiti katika mazao hayo kwa lengo la kuboresha uzalishaji unaowanufaisha wakulima hasa wadogo.

Mazao mengine yaliyonufaika ni pamba kupitia bodi ya zao hilo (TCB), ufugaji wa samaki na mbogamboga na matunda.