Mbinu nne za kuwajengea hamasa wafanyakazi wako

Imejengeka dhana kuwa watu hawawezi kufanya kazi kwa ufanisi bila kusukumwa.

Ukitaka mtu afanye kazi basi ni lazima umtishe ajisikie yuko hatarini; umdhibiti ajikute hana namna nyingine isipokuwa kufanya kazi na pale inapotokea hajafikia malengo yaliyowekwa basi mwadhibu vikali ili ‘iwe fundisho kwa wafanyakazi wengine.’

Dhana hii ina matatizo kwa sababu kuu mbili. Mosi, msukumo wa nje hauwezi kuleta tija endelevu katika eneo la kazi.

Mtu aliyeongozwa na msukumo wa nje anaweza kufanya kile kilichokusudiwa lakini msukumo huo hautadumu. Mara nyingi mtu huyu anaweza kuonekana kwenye eneo la kazi lakini hafanyi kile anachotarajiwa kukifanya.

Lakini pili, huwezi kumsukuma binadamu kama unavyofanya kwa punda asiyeongozwa na utashi.

Kadri unavyombana afanye kazi, ndivyo anavyobuni namna ya kukwepa kazi.

Kwa namna hii huwezi kupata vingi kutoka kwa binadamu anayejisikia unamtumikisha kwa faida yako.

Ningependa kuamini, ukiwa kiongozi wa ofisi, kampuni au taasisi, ungependa wafanyakazi wako watie bidii katika kufanya kazi.

Mafanikio yako hayategemei ukubwa wa shinikizo linalomlazimisha mtu kufanya kazi bali namna unavyotengeneza msukumo unaoanzia ndani ya mtu.

Katika makala haya ninauita msukumo huu hamasa.

Hamasa ni shauku inayoanzia ndani ya mtu kumchochea kutekeleza jambo kwa hiari yake mwenyewe.

Hamasa humfanya mtu asisubiri kukumbushwa kufanya wajibu wake.

Mtu aliyehamasika hufanya zaidi ya kile anachotegemewa kukifanya.

Hapa ninapendekeza mbinu nne za kujenga shauku inayowafanya wafanyakazi wako wajitume bila wewe kulazimika kuwafuatilia.

Mazingira bora ya kazi

Huwezi kutegemea watu wafanye kazi kwa ari bila kuwawekea mazingira yanayowawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Hakuna uzalishaji wenye tija unaoweza kufanywa katika mazingira yanayohatarisha afya za watu.

Hakikisha watu wako wanafanya kazi katika eneo salama lisilohatarisha usalama wao.

Mbali na kufanya juhudi za kuhakikisha eneo la kazi lina vifaa na raslimali zinazohitajika katika kuwawezesha watu kutekeleza wajibu wao kikamilifu, unao wajibu wa kushughulikia kero za watu wako.

Weka mfumo mzuri wa kupokea na kutatua shida zinazowakabili watu wako.

Wafanye waamini changamoto ambazo hazijatatuliwa bado zinatambuliwa na zinafanyiwa kazi kadri uwezo unavyoruhusu.

Usitegemee watu wanaweza kuwa na ari ya kufanya kazi katika mazingira ambayo wanajua kuna mambo hayaendi sawa.

Pokea mawazo mapya

Wapo viongozi wanaoamini nafasi zao zinawafanya wawe na maarifa kuliko wale wanaowaongoza.

Viongozi wa namna hii huwa hawaambiliki na kupenda kila wanachokifikiri wao kifuatwe.

Wanachosahau ni kwamba kadri unavyomfanya mtu ajione hana fursa ya kusema mawazo yake ndivyo unavyozima hamasa yake.

Fahari ya binadamu anayejitambua ni kuona ana mchango wa kutoa mahali. Unapokwenda kinyume na hitaji hili la kimaumbile unamfanya mtu ajione hana thamani na hivyo hatakuwa na msukumo wa kufanya kitu.

Nafasi ya uongozi haikufanyi uwe mjuzi kuliko wale unaowaongoza.

Tena wakati mwingine unaweza kuongoza watu wanaokuzidi uwezo na busara. Watu hawa wanajua wanakuzidi.

Usipotafuta namna ya kuziba pengo hilo, unaweza kuwafanya watu wakapoteza hamasa ya kazi.

Jifunze kutumia mawazo ya watu unaowaongoza. Bainisha tatizo na wakaribishe watu waseme wafikiri namna ya kulitatua.

Kwa kutambua kuwa mawazo yao yanasikilizwa na kufanyiwa kazi, watu hawa watakuwa na hamasa kubwa ya kufanya zaidi ya vile ulivyotarajia.

Wafanye wajitambulishe na kampuni

Huwezi kutoa kile ulichonacho ndani yako kama huna hakika sana na mustakabali wako kwenye taasisi au kampuni.

Mtu anayejisikia mgeni na mpitaji mara nyingi hataweza kuwa na muda wa kufanya kila kilicho kwenye uwezo wake kwa manufaa ya kampuni au taasisi.

Ndio kusema ukitaka mtu ajitume kutoa ‘dhahabu’ inayoishi ndani yake kwa maana ya kutuma vipaji vyake, uwezo wake, uzoefu wake, tena kwa utashi wake mwenyewe, mfanye ajisikie kuwa sehemu kamili ya taasisi au kampuni.

Tumia lugha inayoonesha kuwa mustakabali wa taasisi au kampuni uko mikononi mwa watu wenyewe. Usijikweze uonekane wewe ndio mhusika mkuu na kwamba bila wewe mambo hayaendi.

Badala ya kusema, ‘Ninataka kuweka historia ya kuwa Mkurugenzi wa kwanza aliyeweza kuzalisha bidhaa zilizokidhi soko la nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara’ badala yake sema maneno kama,

‘Kwa pamoja tunataka ikifika mapema mwakani shirika letu liwe na uwezo wa kukidhi soko la nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.’

Lugha ya kwanza inawafanya watu wajione wanakutumikia wewe na mwisho wa siku wewe ndiye mnufaika mkuu wa sifa.

Lugha ya pili inawafanya watu wajione wao ni sehemu ya mafanikio yanayotafutwa.

Mkakati wa kuwaendeleza watu

Watu hawafanyi kazi kwa minajili ya kupata mshahara mzuri pekee.

Kwamba wakati mwingine watu hufanya kazi zisizolipa lakini kwa moyo maana yake kuna zaidi ya mshahara.

Msukumo mmoja wapo unaoweza kuwafanya watu wajitume kwenye eneo la kazi ni vile wanavyoleta tofauti inayoonekana katika maisha ya watu.

Fikiria daktari anayelipwa mshahara wa kawaida lakini anasikia utoshelevu anapotathmini namna kazi yake inavyookoa maisha ya watu wengine.

Mtu kama huyu anahitaji kujiendeleza kiujuzi ili aweze kufanya kazi yake kwa umahiri zaidi.

Anapojisikia udumavu, kutokukua kiujuzi, inakuwa rahisi kwake kupoteza ari ya kazi.

Mwekee mfanyakazi mazingira ya kuamini kuwa una mpango unaoeleweka wa kumwendeleza kiujuzi na hivyo kuongeza ari yake ya kazi.

Hata katika mazingira ambayo uwezo wako wa kifedha hauruhusu, angalau uoneshe kujali.

Mikopo kwa wafanyakazi; utaratibu wa kutoa ruhusa ya masomo; kuwaunganisha na mitandao ya ufadhili wa masomo pamoja na kuwapeleka kwenye mafunzo ya muda mfupi, hizi ni baadhi ya hatua zinazoweza kujenga hamasa ya kazi.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya Simu: 0754870815