Mbio zamponza diwani Geita

Dereva Sylvester Mahendeka wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, akitoa maelezo kwa Mkuu wa Polisi wa wilaya hiyo, Ally Kitimbu baada ya askari kuvunja kioo cha gari hilo.

Muktasari:

  • Madiwani wawili wanashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Geita kutokana na mgogoro unaoendelea kati yao na GGM.

Geita. Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Hadija Said amekamatwa baada ya kuanguka akiwakimbia polisi.

Polisi wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi na madiwani waliofunga  barabara ya kuingia kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) leo Alhamisi asubuhi.

Madiwani wa halmashauri mbili za Wilaya ya Geita jana Jumatano walitanga mgogoro na GGM wakishinikiza kulipwa Dola 12 milioni za Marekani zinazotokana na ushuru wa huduma kuanzia mwaka 2004 hadi 2013.

Walitangaza kuzuia magari ya mgodi kwa kufunga barabara na pia kufunga maji yanayoingia mgodini kutoka Ziwa Victoria.

Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Costantine Morandi ameiambia Mwananchi kuwa mwingine anayeshikiliwa na polisi ni Martin Kwilasa ambaye ni diwani wa Bung'wangoko.

Polisi hivi sasa wameimarisha ulinzi kwenye maeneo ya Nungwe uliko mradi wa kusambaza maji mgodini, eneo la uwanja wa ndege na geti la kuingia mgodini.

Wakati huohuo, gari alilokuwa amepanda makamu mwenyekiti wa halmashauri, Said limevunjwa kioo na polisi.

Dereva wa gari hilo, Sylvester Mahendeka akitoa maelezo kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Geita, Ally Kitimbu baada ya kioo cha upande wake kuvunjwa amesema akiwa amesogeza gari pembeni kumsubiri Said alifika askari aliyemtaka alitoe eneo hilo.

Gari la Halmashauri ya Wilaya ya Geita lililovunjwa kioo na polisi leo.

Said amesema alimweleza askari huyo kwamba anamsubiri makamu mwenyekiti ndipo alipokipiga kwa kirungu kioo cha upande wake na kukivunja.

Hivi sasa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Ezekiel Kyunga, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Mponjoli Mwabulambo na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya wapo mgodini kwa mazungumzo.