VIDEO: Mbivu na mbichi Miss Tanzania ni leo

Muktasari:

Washiriki hao 20 kutoka katika kanda sita nchini watachuana kuwania taji hilo kubwa na kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa ya Miss World.


Taji la Miss Tanzania leo litahama kutoka kwa Julieth Kabete na kwenda kwa mmoja kati ya warembo 20 wanaochuana kurithi kiti hicho kikubwa cha ulimbwende nchini.

Fainali za mashindano hayo zitafanyika Septemba 8, katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano ya kimataifa wa Mwalimu Nyerere(JNICC).

Washiriki hao 20 kutoka katika kanda sita nchini watachuana kuwania taji hilo kubwa na kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa ya Miss World.

Mbali na taji hilo kubwa, Meneja Masoko wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mariam Kobelo amesema Wizara ya Maliasili na Utalii imeamua kuwatumia warembo hao kuwa mabalozi wa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini. Ametangaza kuwa mwaka huu warembo watano wa watakaoibuka kidedea kwenye shindano hilo watavikwa mataji ya ubalozi ikiwemo Miss Domestic Tourism, Miss Ruaha, Miss Ngorongoro, Miss Selous na Miss Eco Tourism.

Ahadi za warembo

Washiriki wameonyesha nia ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili kulifanya pato linalotokana na sekta hiyo kuongezeka maradufu. Dhamira hiyo ya warembo hao imeonekana baada ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo katika mkoa wa Tanga.

Warembo hao 20 walizuru mapango ya Amboni na hifadhi ya msitu wa asili wa Amani wenye vivutio vingi vya kipekee.

Baadhi ya vivutio vilivyowavutia ni pamoja na safu za milima Usambara, maporomoko ya maji, vinyonga wa pembe tatu, maua ya mwituni ya St Paulia na mashamba ya chai.

Baadhi ya warembo hao waliliambia gazeti hili kuwa hapo awali hakuwahi kujua kuhusu vivutio hivyo ila wanatamani vifahamike zaidi.

Mshiriki kutoka kanda ya Ziwa, Mariam Mmari alieleza kuwa bado kuna Watanzania wengi hawafahamu utajiri wa vivutio walivyonavyo katika nchi yao.

Akijitolea mfano yeye alisema alikuwa hafahamu chochote kuhusu hifadhi ya msitu wa amani ambao una vivutio lukuki.

“Binafsi sikuwa nafahamu chochote nimejifunza, nimeona vingi ambavyo hata nilikuwa sivijui.

“Kuanzia hapa nitatumia nafasi yangu ambayo ninayo kutangaza msitu huu, ni utalii mzuri mno kwa watu wote wa ndani na nje ya nchi,” Naye Miss Arusha Teddy Mkenda alisema ipo haja ya serikali kuongeza nguvu katika kuvitangaza vivutio vya utalii ambavyo havifahamiki. “Wengi tumezoea mbuga za wanyama au utalii wa fukwe kumbe kuna utalii wa misitu unaohusisha mimea na viumbe mbalimbali wakiwemo vipepeo wa kipekee ambao tunaweza kusema tunajivunia kama nchi kuwa nao.”