Mbowe alazwa KCMC saa 24, wenzake waripoti polisi

Katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji (aliyenyanyua mkono juu) na naibu katibu mkuu wa chama hicho (Bara), John Mnyika wakitoka kuhojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Ofisa habari wa Hospitali ya KCMC, Gabriel Chisseo alithibitisha kuwa Mbowe aliyekuwa amelazwa juzi saa mbili usiku, aliruhusiwa jana saa moja usiku.

Moshi/Dar. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe jana aliruhusiwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya KCMC baada ya kulazwa kwa saa 24.

Ofisa habari wa Hospitali ya KCMC, Gabriel Chisseo alithibitisha kuwa Mbowe aliyekuwa amelazwa juzi saa mbili usiku, aliruhusiwa jana saa moja usiku.

Awali Chadema walisema wameimarisha ulinzi na hawakutaka mtu yeyote kuingia kumjulia hali bila kibali maalumu kutoka kwao.

Hali ilivyokuwa

Mbowe, ambaye jana alipaswa kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam, aliugua ghafla juzi usiku akiwa anapata chakula na viongozi wengine katika hoteli ya Keys mjini Moshi kabla ya kuwahishwa KCMC kwa matibabu.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema alisema jana baada ya Mbowe kufikishwa KCMC, madaktari walimwekea oksijeni kumsaidia kupumua lakini iliondolewa baada ya afya yake kuimarika.

“Aliugua ghafla jana (juzi) na alipelekwa KCMC, madaktari walilazimika kumwekea oksijeni ili ku-stabilize (kudhibiti) afya yake lakini baadaye waliiondoa baada ya afya yake kuimarika,” alisema.

Awali jana mchana, Lema alikataa kuingia kwa undani kuhusu ugonjwa unaomsumbua Mbowe akisema suala hiyo ni siri ya mgonjwa na daktari wake ila alikiri kuwa mwenyekiti huyo alipelekwa hospitalini juzi saa mbili usiku.

Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari jana mchana, ofisa habari wa Hospitali ya KCMC, Gabriel Chisseo alisema walimpokea Mbowe juzi akiwa na maumivu makali ya kichwa na kwamba jana alikuwa akiendelea vizuri.

“Jana (juzi) jioni tulimpokea Mbowe na taarifa zetu zinaonyesha alikuwa anaumwa kichwa, taarifa za kitabibu zikaonyesha ni uchovu,” alisema Chisseo na kwamba atafanyiwa vipimo zaidi.

Chisseo alisema madaktari bingwa wanaomhudumia Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni (KUB) wameelekeza kiongozi huyo apate muda mrefu wa kupumzika.

Hata hivyo, ipofika saa moja jioni, Chisseo alisema wamemruhusu Mbowe kutoka hospitali baada ya kupata nafuu.

Awali Chadema walisema wangeimarisha ulinzi katika wodi ya watu mashuhuri (VIP) alikokuwa amelazwa kiongozi huyo.

“Hatutaruhusu mtu yeyote kuingia katika wodi aliyolazwa Mbowe bila kwanza kujiridhisha ni nani na kama ni mtu mwema. Wananchi watakaopata nafasi ya kumjulia hali watapewa vibali maalumu,” alisema Lema kabla ya Mbowe kuruhusiwa jana usiku.

Lema alisema baada ya Mwananchi kuandika habari ya kuugua Mbowe na kuiweka mtandaoni (MCL Digital) alipokea simu nyingi kutoka ndani na nje ya nchi wakimtakia heri apone haraka.

Viongozi Chadema waripoti polisi

Kutokana na hali hiyo, Mbowe jana alishindwa kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam kama alivyotakiwa awali.

Katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji ndiye aliyewaongoza viongozi wengine wa Chadema kuripoti kituoni hapo walikofika saa mbili asubuhi.

Mbali na Mashinji, viongozi wengine waliofika kituoni ni manaibu katibu wakuu wa Chadema, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).

Wengine ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee, mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, John Heche na Esther Matiko ambaye ni mweka hazina wa Bawacha.

Februari 27, viongozi hao wakiongozwa na Mbowe walifika kituoni hapo na kuhojiwa kwa takriban saa tano, kisha kuachiwa kwa dhamana na kutakiwa kuripoti tena jana. Siku hiyo Mashinji hakufika kwa kuwa alikuwa nje ya nchi.

Lakini jana katibu mkuu huyo alihojiwa peke yake kuanzia saa saa 5:30 asubuhi hadi saa 7:30 mchana, kisha kuachiwa kwa dhamana kwa kosa la kufanya mkusanyiko usio halali.

Viongozi hao walikumbwa na mkasa wa kutakiwa kuripoti polisi Februari 20 baada ya Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuagiza kukamatwa viongozi saba waandamizi wa Chadema akiwamo Mbowe.

Tukio hilo lilitolewa ikiwa ni siku chache tangu polisi wawatawanye wafuasi wa Chadema waliokuwa wakiandamana kwenda ofisi ya mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao.

Katika tukio hilo mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini aliuwa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala.

Akizungumza baada ya kuachiwa jana, Dk Mashinji alisema kuitwa kwake ni mwendelezo kuhusu matukio yaliyotokea wakati wa uchaguzi wa ubunge Jimbo la Kinondoni uliofanyika Februari 17.

Alisema alihojiwa kwa makosa ya kufanya mkusanyiko usio halali wakati wa maandamano ya kwenda kudai viapo kwa mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni.

“Niliulizwa kwa nini baada ya mkutano tulifanya maandamano, niliwajibu tulikuwa tunaongozana na mawakala kwenda kudai viapo vya mawakala wetu kwa mkurugenzi wa Kinondoni baada ya mkutano. Baada ya mahojiano nilipewa dhamana na tumeambiwa turudi Jumanne ijayo,” alisema.

Mmoja wa mawakili wa viongozi hao, Alex Massaba alisema kwa kuwa wameendelea kuitwa bila kufikishwa mahakamani, Machi 13 itakuwa ya mwisho iwapo wataitwa bila kupelekwa mahakamani.

Alisema hawatakwenda tena kwa sababu wanapotezewa muda.

“Wamekuwa wakituita bila kutueleza chochote sasa imekuwa kama kifungo cha nje. Jumanne ijayo itakuwa siku ya mwisho hatutakwenda tena,” alisema.

Alisema viongozi hao wa Chadema wengi ni wabunge, wakiendelea kuripoti polisi watashindwa kutekeleza majukumu yao katika vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge na Bunge la Bajeti vitakavyoanza hivi karibuni.

“Mashinji hakuwepo wakati wenzake wanahojiwa lakini leo (jana) amefika na amehojiwa kwa kosa moja la kufanya mkusanyiko usio halali,”alisema Massaba.

Imeandikwa na Daniel Mjema, Janet Joseph (Moshi), Pamela Chilongola na Fortune Francis (Dar)