Mbowe amtumia rambirambi Rais Magufuli

Muktasari:

Monica alifariki jana asubuhi katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza alikokuwa amelazwa kwa matibabu zaidi.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amemtumia rambirambi Rais John Magufuli kufuatia kifo cha dada yake, Monica.

Monica alifariki jana asubuhi katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza alikokuwa amelazwa kwa matibabu zaidi.

Mbowe pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ameandika katika ukusara wake wa Twitter akisema, “Kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na wana Chadema wote, natoa pole na salaam za rambi rambi kwa Mh. Rais @MagufuliJPM kwa kufiwa na dada yake Monica Magufuli.”

“Mungu awape faraja na ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi,” ameongeza Mbowe

Mwanachama wa Chadema, aliyewahi kuwa waziri katika utawala wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Lazaro Nyalandu ameandika katika twitter yake akisema, “Natoa pole kwa Mh. Rais @MagufuliJP na familia yake kwa kufiwa na dada yake mpendwa, Monica Magufuli.”

“Hakika, Maisha yana thamani kubwa. Mungu awafariji na ampe dada yetu pumziko la milele mahali pema peponi, Amina,” ameongeza Nyalandu

Mwanasiasa mkongwe nchini, Profesa Mark Mwandosya naye ameandika katika Twitter yake akisema, “Familia yangu na mimi mwenyewe tunawapa pole Mheshimiwa Rais @MagufuliJP na familia yote Chato na kwingineko kifo cha mpendwa wenu Bi. Monica Joseph Magufuli.”

Profesa Mwandosya ameongeza, “Mwenyezi Mungu awape subira. Kwake tulitoka na hakika tutarudi Kwake. Raha ya milele umpe Ee Bwana. Apumzike kwa Amani.

Waziri wa zamani wa maliasili na utalii, Balozi Khamis Kagasheki kupitia Twitter amesema, “Mh Rais Magufuli @MagufuliJP nakupa mkono wa pole wewe na family yako kwa kuondokewa na dada yako Bi Monica. Apumzike kwa amani.”

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umetoa rambirambi ukisema, “Pole kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Joseph Magufuli kwa kuondokewa na dada yake mpendwa Bi. Monica Joseph Magufuli.”

“Bwana ametoa na Bwana ametwaa, Jina la Bwana lihidimiwe. Apumzike kwa Amani,” umeongeza