Mbowe apelekwa nje ya nchi kwa matibabu

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameshindwa kufika mahakamani kwa kuwa amesafirishwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameshindwa kufika mahakamani kwa kuwa amepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Imeelezwa kuwa Mbowe anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo na shinikizo la damu.

Kauli hiyo imetolewa mahakamani hapo leo Alhamisi Novemba Mosi, 2018 na mdhamini wa Mbowe, Grayson Celestine aliyedai kuwa amepewa taarifa za ugonjwa wa Mbowe na mke wa mwanasiasa huyo.

Kufuatia maelezo  hayo, wakili wa Serikali mkuu, Faraja Nchimbi ameiomba mahakama kutoa amri ya kumkamata Mbowe ili ajieleze kwa nini dhamana aliyopewa na mahakama isifutwe kwa kushindwa kufika mahakamani.

Nchimbi alitoa maelezo hayo mbele ya hakimu mkazi mkuu, Wilbard Mashauri mara baada ya washtakiwa wanane kupanda kizimbani na Mbowe ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya jinai namba 112, 2018 kukosekana.

Wakili wa Mbowe, Peter Kibatala alianza kwa kuiarifu mahakama kuwa mdhamini wa mwanasiasa huyo yupo mahakamani hapo.

Akitoa maelezo hayo, Celestine amesema jana aliwasiliana na mke wa Mbowe na kumfahamisha kuwa kiongozi huyo wa kambi rasmi ya upinzani bungeni  amesafirishwa kwa ajili ya matibabu ya dharura kutokana na matatizo ya moyo na shinikizo la damu.

"Kwa mujibu wa maelezo ya mkewe, Mbowe anasumbuliwa na moyo na presha (shinikizo la damu)  na familia imemsafirisha kwa dharura  lakini mimi sijaonana naye" amesema Celestine.

Baada ya kueleza hayo, hakimu Mashauri amemuuliza kama ana chochote cha kuithibitishia mahakama kuwa Mbowe amesafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Celestine aliieleza mahakama kuwa mshtakiwa akirejea atawasilisha nyaraka za safari na matibabu, kwamba anaendelea kufanya mawasiliano ili azitume nyaraka kwa njia ya mtandao.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo wakili Nchimbi amedai mdhamini hajaonyesha uzito wowote kwa kuwa hajaeleza Mbowe amekwenda nje ya nchi lini, katika taasisi gani na nchi gani.

“Labda aliondoka akiwa mahututi lakini waliomsindikiza wangeweza  kumdhamini. Sisi upande wa mashtaka hiyo tunaona ni mwendelezo wa dharau ya mshtakiwa namba moja ambaye ni Mbowe kwa mahakama kwa kuwa alishapewa onyo,” amesema Nchimbi.

Nchimbi amesema Mbowe ameamua kwa utashi wake kukiuka amri ya mahakama.

Hata hivyo, hakimu Mashauri amesema iwapo mshtakiwa hatopeleka kielelezo atatoa amri ya kumkamata ili ajieleze kwa nini asifutiwe dhamana kwa kukiuka  masharti ya dhamana aliyopewa na mahakama.

Soma zaidi: