VIDEO- Mbowe ataja mambo manne yaliyomlaza saa 24 Muhimbili

Muktasari:

Kazi nyingi ni pamoja na maandalizi ya mazishi ya kaka yake pamoja na kuandaa hotuba ya bajeti ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, amesema Mbowe.

Dar es Salaam. Msongo wa mawazo, msiba, kazi nyingi na uchovu kupita kiasi ndivyo vilivyosababisha mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuanguka ghafla na baadaye kulazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa takribani saa 24.

Kazi nyingi ni pamoja na maandalizi ya mazishi ya kaka yake pamoja na kuandaa hotuba ya bajeti ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, amesema Mbowe.

Mbowe alilieleza Mwananchi jana mara baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali kuwa alifanya kazi usiku na mchana akiandaa hotuba ya bajeti ya Kambi Rasmi ya Upinzani na akafiwa na kaka yake anayeitwa Henry.

Mbowe alianguka ghafla saa tisa usiku wa kuamkia juzi akiwa nyumbani kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya kuruhusiwa hospitalini hapo, Mbowe alisema kilichokuwa kikimsumbua ni msongo wa mawazo na uchovu kupita kiasi.

“Lakini kwa sasa afya yangu ipo imara, madaktari wangu waliniangalia vyema,” alisema.

Alisema tatizo lake lilisababishwa na msongo wa mawazo na uchovu kutokana na kufanya kazi usiku na mchana.

“Juzi nilitoka Dodoma, kwanza ilikuwa nakuja (Dar es Salaam)kwa ajili ya kesi inayotukabili viongozi wa Chadema. Nikiwa njiani nikapata taarifa za msiba wa kaka yangu na kimsingi upo nyumbani kwangu,” alisema.

“Ukiacha hayo kwa muda mrefu tunafanya kazi bila kupumzika. Tulikuwa tunatayarisha hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kazi ambayo imechukua muda mwingi.

“Leo (jana) nimeruhusiwa narudi nyumbani baada ya msiba nitaendelea na vipimo vingine ambavyo nitaangalia nifanyie ndani au nje ya nchi kulingana na madaktari wangu watakavyoona.”

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema aliliambia Mwananchi juzi kuwa alipata taarifa za msiba wa kaka yake anayeitwa Henry Aikaeli Mbowe akiwa njiani kurudi Dar es Salaam.

Mrema alisema Mbowe alipofika jijini Dar es Salaam aliendelea na vikao vya maandalizi ya msiba wa kaka yake kwa ajili ya kupanga taratibu za mazishi.

“Lakini akiwa katika vikao hivyo alikuwa akilalamika kuishiwa nguvu na baada ya muda ndipo alipoanguka saa 9:00 usiku,” alisema.

Mrema alisema gari la wagonjwa lilimchukua na kumpeleka Muhimbili alfajiri hiyo.